Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula amefunga
mafunzo ya kijeshi wa askari wa jeshi la
uhifadhi 298 yaliyofanyika kwa muda wa miezi 6 katika kituo cha mafunzo ya
jeshi la Uhifadhi Mlele Mkoani Katavi.
Mafunzo ya askari hao 298 yamehusisha taasisi tatu za
uhifadhi ambazo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) yenye askari 81, Wakala
wa huduma za Misitu (TFS) wenye askari 96 na Mamlaka ya usimamizi wa
Wanyamapori (TAWA) yenye askari 121.
Akitoa taarifa ya mafunzo hayo jana Mkuu wa Mafunzo hayo
Kanali Henry Komba ameeleza kuwa mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 1 Oktoba 2023
askari wamefundishwa mada mbalimbali zikiwemo usalama wa habari na
mawasiliano, ukamataji wa wahalifu,
upelelezi, amri za jumla za Jeshi la Uhifadhi, itifaki za kijeshi, uzalendo,
usomaji wa ramani, utalii na huduma kwa wateja pamoja na matumizi ya silaha
mbalimbali.
Naibu Katibu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna wa Polisi
Benedict Wakulyamba amewaelekeza askari
waliohitimu mafunzo kuhakikisha wanajituma kulinda maliasili, kupambana na
wahalifu na kuzingatia misingi ya sheria,
kanuni na haki za binadamu katika ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na
misifu.
Akifunga mafunzo hayo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhe. Dunstan Kitandula amewaelekeza askari wote waliohitimu kuishi kwa vitendo
mafunzo waliyoyapata, kujiepusha na utovu wa nidhamu pamoja na vitendo vya
rushwa ili kulinda viapo vyao.
"Pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa katika
kutekeleza majukumu yenu hakikisheni mnazingatia misingi mikuu mitatu ambayo ni
nidhamu, uadilifu na uaminifu," ameongeza Mhe. Kitandula.
Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi NCAA, Afisa Uhifadhi
Mwandamizi Donatus Gadiye amewaasa askari kujiandaa kikamilifu katika ulinzi,
uhifadhi na kukabiliana na vitendo cha kihalifu ikiwemo changamoto za uhalifu
hasa ujangili katika maeneo ya hifadhi ili kuimarisha usalama wa rasilimali za
nchi.
Mafunzo yametolewa na wakufunzi kutoka Jeshi la wananchi,
jeshi la polisi na jeshi la uhifadhi.
0 Maoni