Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mhe. Dkt. Vincent Mashinji
amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA imeendelea kuunga
mkono jitihada za Baba wa Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha elimu inakuwa kipaumbele wilayani
Serengeti.
Dkt. Mashinji ameyasema hayo
jana Februari 01, 2024 wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi
ya maendeleo inayotekelezwa na TAWA kwa kushirikiana na nguvu za wananchi kwa
fedha zinazotokana na shughuli za uwindaji wa kitalii, ziara iliyofanywa na
TAWA wilayani humo.
"TAWA moja kwa moja wameweza kugusa maisha ya wananchi
katika jamii hasa katika masuala muhimu ambayo hata Baba wa Taifa aliyeanzisha
haya Mapori aliyasisitiza, suala la elimu," amesema Dkt. Mashinji.
"Kwa kumuunga mkono Mhe. Rais TAWA wameweza kutujengea
miradi sita ambayo imejielekeza katika Sekta ya elimu," ameongeza Dkt.
Mashinji.
Akibainisha miradi hiyo Mkuu huyo wa wilaya amesema katika
Kata ya Sedeco, vijiji vya Bonchugu na Mbilikiri TAWA wamejenga chumba kimoja
(1) cha darasa huku Kata ya Kyambahi Kijiji cha Bokore wamejenga vyumba viwili
(2) vya madarasa.
Pia katika Kata ya Manchira Kijiji cha Kazi TAWA wamejenga
nyumba moja (1) ya Mwalimu na matundu kumi (10) ya vyoo katika shule ya Msingi
Rwamchanga kikiwemo choo kwa ajili ya watu wenye changamoto ya viungo vya mwili
(walemavu) pamoja na chumba maalumu cha wanafunzi wakike kwa ajili ya
kubadilishia taulo.
Aidha ameushukuru uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii
pamoja na Menejimenti ya TAWA kwa kurejesha rasilimali ambayo ni endelevu na
kuhakikisha kile kidogo kinachopatikana
katika uhifadhi kinarudi mikononi mwa wananchi.
Kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Kyambahi Mhe.
Herman Kinyalire amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Samia Suluhu Hassan kupitia TAWA kwa kuwezesha ukamilishwaji wa miradi mikubwa
minne (4) katika Kata yake ambayo ni madarasa manne (4), vyumba viwili (2) vya
madarasa pamoja na thamani za shule.
Aidha amesema utekelezaji wa miradi hiyo umechangia kwa kiasi
kikubwa kupunguza ujangili katika Kata yake na kuwafanya wananchi waongeze
ushirikiano katika uhifadhi wa wanyamapori kwa kuwa wanaziona faida za moja kwa
moja zinazotokana na shughuli za uhifadhi.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema
TAWA haiwezi kuongelea mafanikio wanayoyapata ikiwa ni pamoja utekelezaji wa
miradi hiyo bila kuhusisha Jitahada za dhati zilizofanywa na Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipocheza Filamu Maarufu
ya Tanzania The Royal Tour ambayo imekuwa chachu ya ongezeko la watalii wa
Uwindaji katika hifadhi mbalimbali zinazosimamiwa na Taasisi hiyo.
Maganja amesema TAWA imekuwa miongoni mwa Taasisi zilizonufaika na matokeo ya filamu hiyo ambapo katika miezi 10 ya awali kwa Mwaka wa fedha 2022/23 TAWA ilirekodi ongezeko la idadi ya watalii kutoka 541 mpaka 692 idadi ambayo ilivunja rekodi.
Na. Beatus Maganja- Serengeti
0 Maoni