Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara - TANAPA
Herman Batiho amekagua bweni la wasichana jana Februari 23, 2024 katika Shule
ya Sekondari Sitalike iliyoko Wilayani Mpanda katika mkoa wa Katavi
linalojengwa na Shirika hilo ili kuwaondolea wanafunzi wa kike vishawishi
vinavyosababisha mimba walivyokuwa wanakumbana navyo nyakati za kwenda shule na
kurudi nyumbani.
Mradi huo wa bweni unaogharimu kiasi cha shilingi milioni
187.6 umekamilika kwa asilimia 99 huku
ukiwa na vyumba 20 vyenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80, matundu 5 ya vyoo na
mabafu 5 yaliyomo ndani ya bweni hilo, huku asilimia 1 iliyobaki ni uingizwaji
umeme unaotarajiwa kufanywa siku za usoni.
Kamishna Batiho alisema, "Wanafunzi wa kike wamekuwa ni
wahanga wakubwa kutokana na vishawishi wanavyokutana navyo barabarani hivyo
ujenzi wa bweni hili utaondoa adha hiyo na kuwafanya mabinti hawa wapate muda
mwingi wa kujisomea na hatimaye kutimiza ndoto zao."
Naye, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo Anna Lupembe alisema,
"Ninaishukuru TANAPA kwa ujenzi wa bweni hili la kisasa na pia niliwaomba
kutufanyia (wiring) katika nyuma za walimu wa shule ya Sekondari Sitalike,
mkatekeleza."
Mkuu wa shule ya Sekondari Sitalike Mwl. Gervas M. Salehe
alidokeza kuwa hapo awali wanafunzi wetu walikuwa wakikabiliwa na mimba
zilizowapelekea kuacha shule kwa sababu ya kupanga maeneo yenye vishawishi na maeneo hayo kukosa ulinzi kwa watoto wa
kike na kuondoa ari ya kujisomea. Hali hii ilishusha kiwango cha elimu kwa
kiasi kikubwa, ili kuwanusuru wanafunzi hao walimu waliitisha kikao cha wazazi
na kukubaliana baadhi ya vyumba vya madarasa vitumike kama hostel na wazazi
wachangie chakula, baada ya kufanya hivyo utoro ulipungua na ufaulu uliongezaka
maradufu.
"Kulingana na madarasa hayo kutokukidhi vigezo vya kuwa
mabweni kwa kukosa vitanda, ikabidi hostel hizo zifungwe, tokea hapo matokeo ya
wanafunzi yameshuka sana, niwashukuru TANAPA kwa kuiona changamoto hii na
kuifanyia kazi, nina imani mradi ukikamilika siku chache zijazo hata ufaulu utakuwa ni mzuri sana," aliongeza
Mwalimu huyo.
Baada ya ukaguzi wa mradi huo Kamishna Batiho pia, alifanya
kikao na Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Katavi na kuwataka watumishi hao kuwa
wabunifu katika utangazaji wa utalii na kuibua mazao mapya ya utalii ili
kuvutia watalii wengi zaidi.
Hata hivyo, Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini - TANAPA Steria Ndaga, alimshukuru kwa ujio wake na kumuahidi maagizo yote aliyoyatoa kuyafanyia kazi ili kuboresha utendaji kazi na kuongeza fursa za utangazaji kupitia vyombo mbalimbali vya habari na maonesho ya ndani na nje ya nchi ili kuvutia watalii wengi zaidi kuitembelea hifadhi hiyo inayosifika kuwa na viboko wengi.
Na. Jacob Kasiri- Mpanda
0 Maoni