Mbunge wa Jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe
wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Mhe. Geofrey Pinda amekabidhi magari mawili ya wagonjwa kwa halmashauri
ya Mpimbwe iliyopo wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi ili kusaidia kusafirisha
wagonjwa.
Hafla ya kukabidhi magari hayo imefanyika tarehe 3 Februari
2024 katika kituo cha Afya Isevya kilichopo halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya
Mlele na kuhudhuriwa na viongozi wa halmashauri hiyo wakiwemo madiwani.
Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo Mhe. Pinda
alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu
Hassan kwa kuliwezesha jimbo lake katika huduma za sekta ya afya ikiwemo ujenzi
wa vituo vya afya na zahanati.
‘’Nimshukuru Mhe. Dkt
Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia ujenzi wa vituo vya katika jimbo langu, kwa
kweli Mhe. Rais ameifanya Mpimbwe istawi,’’ alisema Mhe. Pinda.
Ameitaka halmashauri ya Mpimbwe na Kituo cha Afya cha Isevya
kuhakikisha magari aliyoyakabidhi yanatunzwa vizuri sambamba na kutumika kwa
yale malengo yaliyokusudiwa ya kuwahudumia wananchi wa Mpimbwe.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa jimbo la Kavuu, wakati anaingia
madarakani mwaka 2020, vituo vya afya kwenye jimbo lake vilikuwa viwili na
kuvitaja kuwa ni kile cha Usevya na Mamba.
Hata hivyo, ameweka wazi kuwa, kwa sasa katika jimbo lake
vimeanzishwa vituo vingine vitatu vya Majimoto, Kibaoni, Kasansa Pamoja na
Zahanati ya Mwamapuli inayokwenda kuanza kazi.
Amesema, ataendelea na juhudi mbalimbali za kuimarisha huduma
za sekta ya afya katika jimbo la Kavuu kwa kuwa afya ni muhimu huku akiwaahidi
wananchi wa jimbo lake kupambana kwa hali na mali ili jimbo hilo libadilike
kimaendeleo na pale atakapomaliza muda wake aache alama itakayomfanya aendelee
kukumbukwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Shamimu
Mwariko amesema, jukumu la halmashauri yake ni kuhakikisha magari
waliyokabidhiwa yanaenda kusaidia na kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa
Mpimbwe.
‘’Tutayalinda na kuhakikisha muda wote yanafanya kazi
iliyokusudiwa ya kusaidia na kuboresha huduma kwa wananchi,’’ alisema Shamimu.
‘’Nimshukuru Rais kwa kuhakikisha huduma zote za afya nchini
ikiwemo Mpimbwe zinakaa vizuri na katika mwaka huu wa fedha halmashauri yetu
inaenda kukamilisha vituo vyetu vya afya vitatu vya Majimoto, Kasansa na
kibaoni kwa asilimia mia moja’’ Alisema.
Mhe. Pinda alikuwa jimboni kwake kwa ziara ya siku moja
ambapo mbali na hafla ya kukabidhi magari ya wagonjwa aliwatembelea na
kuwafariji wananchi wa jimbo lake waliopatwa na ugonjwa wa kipiundupindu katika
eneo la Mwamapuli.
Na. Munir Shemweta- WANMM Mpimbwe
0 Maoni