Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe
Geophrey Pinda amewafunda watendaji wa sekta ya ardhi katika jiji la Mwanza kwa
kuwataka kusimamia sekta hiyo kwa kuzingatia kanuni, taratibu na miongozi ya
sekta hiyo.
Amesema, kwa kufanya hivyo Wizara ya Ardhi itaweza kuepukana
na migogoro ya ardhi isiyo na lazima aliyoieleza kuwa imeendelea kuibuka kila
kukicha katika maeneo mbalimbali.
Mhe. Pinda alisema hayo tarehe 29 Januari 2024 alipokutana
na wakuu wa idara na vitengo wanaosimamia sekta ya ardhi katika Halmashauri ya
Jiji la Mwanza pamoja na wale wa Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa
Mwanza akiwa katika ziara yake mkoani humo.
"Ninyi ndio wasimamizi wa sekta hii ya ardhi katika
jiji la Mwanza hivyo mnao wajibu mkubwa wa kufuata kanuni, taratibu na miongozo
ya sekta hii ili kuepusha migogoro ya ardhi," alisema Mhe. Pinda.
Amewataka wakuu hao wa idara na vitengo kuwa washauri wazuri
wa wakurugenzi wa halmashauri zao ikiwemo kuzishauri halmashauri kuwa na benki
za ardhi katika maeneo yake.
"Ninachotaka kuwaambia silka yangu ni kuwapitisha
katika maeneo mnayoyasimamia na hii itawasaidia kutekeleza majukumu yenu kwa
ufasaha," alisema Mhe. Pinda.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi amehimiza suala la upendo
miongoni mwa watumishi wakati wote wa utendaji kazi kwa kuwa ndiyo njia pekee
ya kuwawezesha wakuu hao wa idara na vitengo kufanya kazi bila kulaumiwa.
Vile vile, Mhe. Pinda amewataka wakuu wa idara na vitengo
katika sekta ya ardhi kuwa na mipango madhubuti itakayofanikisha kuzuia ujenzi
holela pamoja na kuhakikisha maeneo ya wazi yanalindwa.
Amewaasa watendaji hao kuhakikisha wanatatua mgogoro ya
ardhi katika maeneo yao kwa busara ikiwemo kufanya vikao vya kumaliza tofauti
kwa amani.
Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza
Happiness Mtutwa alimshukuru Naibu Waziri wa Ardhi kwa kuwafunda na kuwapa
elimu na maelekezo na kusema hilo ni jambo muhimu sana katika kuiboresha sekta
ya ardhi.
Alisema wao kama wakuu wamepokea maelekezo na namna ya
kuyashusha kwa watumishi wa chini ili mwisho wa siku maeneo wanayoyasimamia
yawe salama.
"Nikutoe hofu mhe waziri ofisi ni taasisi na mara
nyingi tumekuwa tukifanyia maelekezo tunayopatiwa na nikuahidi kutekeleza
maelekezo na ushauri ulioutoa kwetu kwa kuwa ndiyo msingi wa kuiboresha sekta
ya ardhi nchin,” alisema Happy.
Na. Munir Shemweta WANMM- Mwanza
0 Maoni