Madaktari bingwa wabobezi wa China kuhudumu Muhimbili miaka miwili

 

Hospitali ya Taifa Muhimbili imepokea madaktari bingwa bobezi kutoka China ambao watahudumu kwa muda wa miaka miwili katika Idara ya Usingizi na Ganzi, Upasuajiwa Watoto pamoja na Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalum (ICU).

Akizungumzia ujio wa madaktari hao Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi amesema kuwa kutokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na China, Hospitali imekuwa ikipokea wataalam mbalimbali kutoka nchini humo kwa lengo la kutoa huduma na kubadilishana uzoefu.

“Uhusiano ulipo baina ya nchi hizi mbili ni wa muda mrefu takribani miaka 60 ambapo ulianzia kwenye siasa na sasa umekuja hadi kwenye huduma za afya leo tumepokea madaktari watatu ambao watasaidia katika kuendelea kuboresha utoaji wa huduma na kujengeana uzoefu, ”amesema Prof. Janabi.

Pamoja na hayo amesema kuwa China ni nchi ambayo iko mbele zaidi kwenye maendeleo hasa kwenye huduma za afya hivyo kupitia uwepo wao wataalamu wataalamu watajifunza mambo mengi kutoka kwao.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Tiba Asili na Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Vumilia Luggyle amesema kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwanye miundo mbinu ya hospitali ikiwemo vifaa tiba vya kisasa hivyo kupitia wataaam hao watasaidia katika kuboresha huduma za afya nchini.

“Tunaamini kushirikiana na China katika eneo la huduma za tiba wananchi wanaohitaji huduma za kibingwa na ubingwa bobezi watanufaika kwa kuwa madaktari wetu watapata uzoefu,” amesisitiza Dkt.Luggyle.

 Hospitali ya Taifa Muhimbili imekuwa ikipokea watalam mbalimbali kutoka nchi zilizoendelea kwa lengo la kubadilishana uzoefu baina ya wataaam hao kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma za afya na kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa wananchi.

Chapisha Maoni

0 Maoni