Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki
amewaalika wawekezaji kutoka Marekani na duniani kwa ujumla kuja kuwekeza nchini
katika sekta ya Utalii na sekta nyingine kwa kuwa Tanzania imebarikiwa
raslimali za kutosha na uongozi bora wa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu
Hassan.
Mhe. Kairuki ametoa rai hiyo kwenye hafla maalum ya
kuukaribisha ujumbe wa mabilionea kutoka Marekani wakiongozwa na Mchezaji namba
moja duniani na mtu anayetambulika kama “Pele” au “Mohammed Alli” wa Tenesi
duniani, John McEnroe na mdogo wake Patrick ambao wamekuja nchini za wenzao
zaidi ya 70 kutalii lakini pia kushiriki tukio la kihistoria la kucheza tenesi
(#TennisInSerengeti) Desemba 5 mwaka huu katikati ya Hifadhi ya Serengeti.
Amesema sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa
kasi hapa nchini na duniani kwa ujumla ambapo amesema programu ya filamu ya
"The Royal Tour" iliyochezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa mikakati iliyosaidia
kukua kwa utalii hapa nchini.
Akifafanua amesema matokeo chanya ya The Royal Tour ni
pamoja ongezeko la watalii kutoka nje ambapo waliongezeka kutoka watalii
milioni 1.3 Oktoba 2022 hadi kufikia watalii milioni 1.7 Oktoba 2023.
Aidha, amesema Sera ya
Utalii ya mwaka 1999 inasisitiza ushirikishwaji madhubuti wa wadau wote kwenye
mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii ambapo amesema Serikali itaendelea
kuzingatia ushirikishwaji huo na amepongeza Kampuni ya Insider Expeditions na
Gosheni Safari kwa kushirikiana kuwaleta wageni hao kupitia program ijulikanayo
kama EPIC Tour ambapo mwanzoni mwa Novemba mwaka huu iliwaleta watalii
mabilionea zaidi ya 150.
Ametaja baadhi ya maeneo yenye fursa ya uwekezaji kwenye
mnyororo wa thamani kwenye sekta ya utalii kuwa ni pamoja na makazi, kumbi za
mikutano, usafirishaji wa wageni, ujenzi wa mahoteli na utalii wa bahari kwa juapande
wa Tanzania bara na Zanzibar
Pia Mhe. Kairuki amesema amefafanua kuwa katika kuhakikisha
kuwa sekta ya Utalii inaendelea kukua, Serikali imejikita katika kuboresha
miundombinu ya Reli ya Kisasa ya SGR ili kuweza kufikia vivutio katika maeneo
mbalimbali nchini, ambapo pia amesema kumekuwa na kuimarishwa na kuongeza
huduma za usafiri wa anga na maboresho kwenye miundombinu ya viwanja vya ndege.
Kwa upande wake na kwa niaba ya ujumbe wa wageni hao John
McEnroe amesema wanashukuru mapokezi mazuri waliyoyapata kutoka Serikali ya
Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii huku akiahidi kuimarisha
uhusiano baina yao na Tanzania.
Amesema wameamua pamoja na lengo la kuja kutalii pia kushirikiana
na Serikali ya Tanzania kuutangaza Utalii wa Tanzania duniani kupitia mchezo wa
tennis na kunyanyua vipaji vya watoto.
Mara baada ya kuwasili jijini Arusha leo wamefanya program maalum
ya kuwafundisha na kucheza na vijana mchezo wa tenesi.
Hafla hiyo imepambwa na vikundi mbalimbali vya Sanaa kama
Wanne Star na Sholo Mwamba na kukonga nyoyo za wageni hao ambao hawakusita
kupanda jukwaani.
Na. John Mapepele
0 Maoni