Watumishi 22 TANAPA watunukiwa medali kwa kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro

 

Kaimu Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA, Juma Kuji amewavisha medali watumishi 22 wa Shirika la Hifadhi za Tanzania waliofika katika kilele kirefu zaidi barani Afrika cha Mlima Kilimanjaro chenye urefu wa mita 5895 kutoka usawa wa Bahari kwa lengo la kusheherekea kumbukizi ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika wakati wa kampeni ya "Twenzetu Kileleni 2023"  leo tarehe 27.12.2023 katika Ofisi za Makao Makuu ya TANAPA yaliyopo jijini Arusha.

Akitoa pongezi kwa maafisa na askari hao, Kamishna Kuji alisema, "niwapongeze sana kwa kuliheshimisha Shirika kwa kufanikiwa kufika katika kilele hiki ambacho ni kivutio kikubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Kufika kwenu kumeonyesha nia na adhma yenu katika kushiriki zoezi hili lililloshirikisha  waheshimiwa Mabalozi na taasisi nyingine nyingi zilizojumuisha watanzania zaidi ya 200 waliopitia njia tatu tofauti".

Aidha, Kamishna Kuji aliongeza kuwa kwa mwaka unaokuja 2024 maafisa na askari wajitokeze kwa wingi ili kuiheshimisha Wizara ya Maliasili na Utalii na TANAPA kwa ujumla ili mfike wengi zaidi tofauti na ilivyokuwa kwa mwaka huu 2023.

Vile vile,  Kamishna huyo aliwataka watumishi wake waanze kampeni ya "Twenzetu Kileleni seasion (4), 2024"  ianze mapema ili kuhamasisha na kuvutia watanzania wengi zaidi. "Kamishna Kuji alisema, Mhe. Angellah Kairuki - Waziri wa Maliasili na Utalii ametutaka mwakani kampeni hii iwe na watanzania 500 wakipanda katika Malango tofauti hivyo ni jukumu letu kufanikisha lengo hili la waziri."

Afisa Uhifadhi Mkuu - TANAPA kutoka kitengo cha Maendeleo ya Biashara Makao Makuu, Augustine Masesa alisema kuwa lengo la kuwavisha medali ni kutambua mchango wa watumishi hao na kutoa hamasa kwa watumishi wengine kujitokeza kupanda Mlima Kilimanjaro na kufika katika kilele hicho, kwani kupanda mlima huo sio kazi rahisi inahitaji kujituma na uvumilivu.

Zoezi la kuwavisha medali hizo limefana sana kwani maafisa na askari hao wamemshukuru sana Kaimu Kamishna huyo na kuahidi kushiriki tena mwakani wakati wa kupandisha Bendera ya Taifa ili kusheherekea kumbukizi ya miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika.

Na. Philipo Hassan, Arusha

Chapisha Maoni

0 Maoni