Wazambia waja nchini kujifunza mbinu za kukabiliana na ujangili

 

Timu ya Maafisa Wandamizi kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Zambia vinavyohusika na uzuiaji ujangili wamefika nchini kwa lengo la kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa katika mapambano dhidi ujangili. Timu hiyo iko nchini kwa siku tano kuanzia Oktoba 29 hadi 4 Novemba, 2023.

Akizungumza mara baada ya kutembelea Hifadhi ya Ziwa Manyara, Kamishna wa uzuiaji ujangili nchini Zambia, Brigedia Jenerali, Herman Kamwita ambaye ni kiongozi wa ujumbe wa Zambia alisema wamekuja kuona namnaTanzania ilivyofanikiwa kuendesha operesheni za kupambana na ujangili na utekelezaji wa Mkakati wa Kupambana na Ujangili.

Alisema Kamisheni ya kudumu ya Tanzania na Zambia ya Ulinzi na Usalama ilipendekeza Mamlaka ya nchi hizo mbili kuwa na utaratibu wa kubadilisha uzoefu katika kulinda rasilimali za wanyamapori na misitu.

Alisema wameweza kupitishwa katika mbinu mbalimbali ambazo Tanzania inatumia katika kupambana na ujangili na kuwa wamepanga kwenda kuzitumia wakirudi nchini kwao.

Aliongeza kuwa, "tumepata fursa ya kwenda Hifadhi ya Ziwa Manyara na tumeona wanyama mbalimbali na hii imedhihirisha namna wenzetu walivyopiga hatua kwenye uhifadhi na niwahakikishie kuwa tutakwenda kutumia mbinu hizi ili kuimarisha sekta ya utalii nchini kwetu.’’

Awali, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Uzuiaji Ujangili na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Taifa Bw. Kiza Yusuph Baraga alisema wamepokea ugeni kutoka Zambia na kuwa kupitia ziara hiyo, pande hizo mbili zimebadilishana uzoefu.

" Madhuni na nia ya nchi yetu ni kuendelea kutangaza utalii hasa kutokana na juhudi zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii kupitia Filamu ya The Royal Tour".

Ugeni huu pia, umepata fursa ya kujionea vivutio vya utalii baada ya kutembelea Hifadhi ya Ziwa Manyara na kushuhudia shughuli mbalimbali za utalii zinazoendelea ndani ya hifadhi hiyo.

Aidha, ugeni huo umefurahishwa na mandhari nzuri na tunu tulizonazo na kuahidi kuwa sehemu ya kutangaza utalii wetu nchini Zambia. Nitoe wito kwa watalii mbalimbali hususani wa ndani na nje ya nchi kuja kutembelea vivutio vilivyopo Tanzania."

Kamanda wa Uhifadhi - Kanda ya Kaskazini, Betrita Lyimo aliishukuru Wizara kwa ugeni huo kwa kutembelea Hifadhi za Taifa Tarangire na Manyara kujionea hazina kubwa tuliojaliwa Tanzania.

Aidha, Wakili Mwandamizi Ofisi ya Mashtaka Makao Makuu ambaye pia ni Mratibu wa upelelezi, uendeshaji wa kesi za makosa ya rushwa, udanganyifu na utakatishaji fedha sehemu ya makosa ya mazingira na maliasili wa Kikosi cha Taifa cha Kupambana na Ujangili Theophil Daniel Mutakyawa alisema, "kupokea ugeni huo na kubadilisha uzoefu ni mwanzo wa ushirikiano katika kupambana na ujangili na pia kubadilishana taarifa zinazohusiana na ulinzi wa Maliasili.

Mutakyawa aliongeza kuwa makosa ya ujangili ni makosa yanayovuka mipaka, hivyo yanahitaji nguvu ya pamoja ya kikanda katika kupambana na uhalifu huo mkubwa.

" Tumezungumza na kuelewana kuwa sasa wanaporudi nchini kwao na sisi kubaki huku, utakuwa mwanzo wa kuendelea kupeana uzoefu na taarifa ili tuweze kupambana na uhalifu mkubwa."

Na John Bera

Chapisha Maoni

0 Maoni