Korea Kusini imeonesha nia yake ya kushirikiana na Hospitali
ya Taifa Muhimbili katika kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba vya uchunguzi vya
kisasa kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya ya utoaji huduma za afya.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Global Cooperation Committee ya
nchini Korea Kusini Bw. Jinil Kim amesema hayo wakati wa kikao na uongozi wa
Muhimbili kilicholenga kushauriana namna ya kushirikiana ili kuleta maendeleo
katika sekta ya afya hususani kwa upande wa vifaa tiba.
Bw. Kim ameeleza kwamba uwekezaji wa vifaa hivyo utaenda
sambamba na kujengewa uwezo wataalamu namna bora ya kutumia vifaa na jinsi ya
kuvifanyia ukarabati ili viweze kutumika kwa usahihi na kudumu kwa muda mrefu.
“Miaka 60 iliyopita Korea Kusini ilikua nyuma sana
kimaendeleo, hivyo tunaamini endapo mkijidhatiti na tukashirikiana vema
ninaiona Tanzania miaka 30 ijayo itakua imepiga hatua kubwa sana kimaendeleo,”
amefafanua Bw. Kim.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Julieth Magandi amesema Tanzania imekua na
ushirikiano mzuri na Korea Kusini tangu enzi za Hayati Baba wa Taifa Mwl.
Julius Nyerere na hadi sasa uhusinao huo unaendelea kukua zaidi.
Ameongeza kuwa Korea Kusini imekua ikiisaidai Tanzania
katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa jengo la Hospitali ya
Mloganzila, kusaidia vifaa tiba pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu
wa ndani.
“Hatuna shaka na vifaa kutoka Korea Kusini kwakuwa vifaa
vingi vinavyotumika MNH Mloganzila vimetoka Korea, bado wanatusaidia katika
maeneo tofauti tofauti hivyo tunathamini mchango wao,” amesema Dkt. Magandi
Dkt. Magandi ameishukuru Korea Kusini kwa kuonyesha nia ya
kuisaidia Muhimbili na kueleza kwamba MNH ipo tayari kushirikiana nao ili
kuhakikisha lengo la kuboresha sekta ya afya linafikiwa kwa mafanikio makubwa.
0 Maoni