Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, amesema
upatikanaji wa Umeme Vijijini kunaimarisha ubora wa elimu kwa shule za Msingi
na Sekondari nchini.
Mhe. Kapinga amesema hayo wakati wa hafla ya kuwasha umeme
kwa mara ya kwanza katika Kijiji cha Ukata wilayani Mbinga wakati wa ziara ya
kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa umeme Vijijini Awamu ya Tatu
Mzunguko wa pili Mkoani Ruvuma.
Amefafanua kwamba nia ya Serikali ni kuhakikisha mazingira
ya ufundishaji na pamoja na ya kusomea kwa watoto wote nchini yanaimarishwa,
pia wazazi wanasomesha watoto kwa jasho kwa mategemeo ya kupata viongozi bora
wa kesho.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunaboresha mazingira ya
ufundishaji ili walimu waweze kutumia vitendea kazi vinavyoendana na ulimwengu
wa Sayansi na Teknolojia, haiwezekani mwalimu asiwe na Kompyuta wala na Printer
akiwa anafundisha ili kusaidia mtoto tutakuwa tunalea taifa la aina gani?
Kwahiyo ni lazima kuweka umeme sababu Dunia nzima inaenda na maendeleo ya
sayansi na teknolojia,” alisisitiza Mhe. Kapinga.
Mhe. Kapinga aliwaeleza wananchi kuwa maendeleo ni hatua
hivyo mradi wa REA unatekelezwa kwa awamu katika vijiji vyote nchini, na
ifikapo Desemba 2023 vijiji vyote vitaunganishwa na umeme na kama kuna
kitakachosalia kitaunganishwa wakati wa kuunganisha vijiji 22024.
Katika ziara hiyo Mhe. Kapinga aliambatana na Viongozi
kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO).
0 Maoni