WAZIRI MKUU Mh. Kassim Majaliwa amepokea taarifa ya
uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwenye Halmashauri ya Manispaa ya
Kigoma Ujiji ambapo imebainika watu 10 wanahusika na mtandao wa uhamishaji
fedha kinyume cha taratibu.
“Taarifa nimeipokea na mapendekezo ya Kamati wote
tumeyasikia. Hatua za haraka zichukuliwe kwa sababu Mheshimiwa Rais anatafuta
fedha za kuleta maendeleo lakini kuna watu wachache wanafanya ubadhirifu,”
amesema Mh. Majaliwa.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo leo (Jumatano,
Oktoba 25, 2023) ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema kila
mtumishi wa umma ni lazima atunze na kuratibu vizuri matumizi ya fedha
zinazopatikana.
Amewataka Mawaziri na Makatibu Wakuu wasiridhishwe na
taarifa za miradi wanazopokea pindi wakiwa ziarani kwani licha ya kuwa kuna
wataalamu wanatoa taarifa nzuri mbele ya viongozi hao, bado kuna tricks
wanachezacheza.
Akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Kigoma, Septemba 20-22,
mwaka huu, Waziri Mkuu alipata taarifa ya uwepo wa fedha zilizoingizwa kwenye
akaunti ya Amana ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kutoka TAMISEMI na
kisha fedha hizo kuondolewa baada ya muda bila maelekezo maalum wala kujua
zilitumikaje.
“Hapa Manispaa mnapokea fedha, zinakaa kwenye akaunti kwa
muda halafu zinapotea, hazijulikani zimefanya nini. Nitaleta timu, waje
wafuatilie hapa Kigoma, waende hadi TAMISEMI ili tuone huo mnyororo unaenda
wapi,” alisema Waziri Mkuu wakati akizungumza na viongozi wa dini, Serikali,
Chama cha Mapinduzi (CCM) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na
Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenye ukumbi wa NSSF, Kigoma mjini Septemba
22, mwaka huu.
Mapema, akitoa taarifa kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa
timu ya uchunguzi, alisema timu hiyo ilibaini kuwa uchepushaji wa fedha hizo
unafanyika kwa kutumia njia kadhaa ikiwemo kuomba kibali kutoka HAZINA cha
kuvuka na bakaa ya fedha za miradi mwaka wa fedha unapokaribia kwisha.
“Timu ya uchunguzi imebaini kuwa jumla ya sh. milioni 463.59
zilitumwa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na hazikuwa kwenye mpango wala
bajeti ya Manispaa na hazijawahi kuombewa matumizi kama bajeti ya ziada,”
alisema.
Aliwataja watumishi waliohusika na uchepushaji wa fedha hizo
kuwa ni Bw. Ferdinand Simon Filimbi, Bw. Salum Juma Said, Bw. Kombe Salum
Kabichi, Bw. Athumani Francis Msabila, Bw. Moses Charles Zahuye, Bi. Jema Linus
Mbilinyi, Mhandisi Joel Langford Shirima, Bw. Aidan Zabron Mponzi, Bi. Tumsifu
Christopher Kachira na Bw. Mzee Mohamed Ubwa. Alisema watumishi hao
wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Alisema mbali ya watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya
Kigoma, wamo pia maafisa kutoka TAMISEMI, HAZINA na baadhi ya wafanyabiashara
ambao wanatumiwa ili kupitisha miamala ya fedha hizo.
Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo alisema kuna ubadhirifu
mkubwa unafanyika kupitia Kitengo cha Usimamizi wa Fedha katika Akaunti Jumuifu
ya Amana kilichopo TAMISEMI. “Timu imebaini kuwa Kitengo cha Usimamizi wa Fedha
katika Akaunti Jumuifu ya Amana kilichopo TAMISEMI kinahusika kutuma fedha
kwenye Halmashauri mbalimbali na kisha kuzitoa kwa kushirikiana na watumishi wa
Halmashauri hizo.”
Alisema baadhi ya Halmashauri zinakuwa hazijaomba kibali cha
kuvuka na fedha za bakaa kutoka HAZINA lakini zinatumiwa fedha hizo, kuna
ambazo zinaomba kibali lakini zinapewa pungufu ya fedha zilizoomba na
zinazobakia hazijulikani zinafanya nini.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni