WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa Wakuu wa
Mikoa yote nchini ambao bado hawajaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi
kiuchumi kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 wawe
wameshaanzisha kabla ya mwaka 2024.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Viongozi na Watendaji
Wakuu wa Taasisi za Umma na Sekta Binafsi waimarishe huduma za uwezeshaji ili
waweze kuyafikia malengo waliojiwekea na kutimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uwezeshaji na kupunguza umaskini nchini.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Oktoba 2,
2023) wakati akifunga Kongamano la Saba la Uwezeshaji Kiuchumi katika ukumbi wa
Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. “Suala la kuanzisha vituo vya
uwezeshaji ni maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka
2020/2025 katika Ibara ya 26 (k) na hili ni jukumu letu viongozi kuhakiksha
ilani inatekelezwa.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaagiza
viongozi wa mikoa na halmashauri zote nchini wahakikishe wanaimarisha Majukwaa
ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika
shughuli za kiuchumi ambazo zitawaongezea kipato.
“Katika hili ninawapongeza Mkoa wa Dodoma kwa kuwezesha
Jukwaa la Mkoa kuanzisha SACCOs 76 za wanawake zenye wanachama 322 pamoja na
Halmashauri ya Ushetu ambayo imeanzisha Jukwaa linaloendesha Mradi wa Kampuni
ya Usafi wa Mazingira na usindikaji wa mboga za majani maarufu kwa jina la
Nsansa.”
Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa alisema kongamano hilo linalenga kuongeza
ufahamu wa wadau mbalimbali kuhusu dhana ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na
kuwakumbusha majukumu waliyonayo katika kuwawezesha Watanzania.
Alisema malengo mengine ni pamoja na wadau kupeana uzoefu
katika kutekeleza shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuzindua taarifa ya
mwaka 2022/2023 ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
ya mwaka 2004 ambayo pia imejumuisha masuala ya ushiriki wa Watanzania katika
miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika nchini.
Katibu Mtendaji huyo alitaja kaulimbiu ya kongamano hilo
kuwa ni “Uwezeshaji kwa Uchumi Endelevu”. “Kaulimbiu hii inaendana na azma ya
Serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha watanzania wanawezeshwa kushiriki
kikamilifu katika uchumi wa nchi ili kuweza kutimiza malengo ya Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2025.”
Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2022/ 2023, mifuko
na programu za uwezeshaji ilifanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi
bilioni 743.7 kwa wanufaika wapatao 6,064,957 ambapo miongoni mwao wanaume ni
asilimia 46 na wanawake asilimia 54.
0 Maoni