Timu ya Afya ya Mkoa wa Dodoma imepongezwa kwa kuendelea
kufanya vizuri katika suala la uchangiaji damu hadi kuvuka lengo la asilimia
100 lililowekwa na kufikia asilimia 110 kwa sasa.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Bi. Ziada Sellah ametoa
takwimu hizo leo Oktoba 03, 2023 jijini Dodoma katika Kituo cha Mikutano cha
Jakaya Kikwete linapofanyika zoezi la uchangiaji damu ikiwa ni moja ya tukio
lililoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
kuelekea Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali litakaofanyika jijini humo
Oktoba 05, 2023.
Bi. Ziada amesema kuwa, suala la uchangiaji damu ni la
muhimu na msingi kwani ni muhimu kuhakikisha damu na mazao ya damu yanakuwepo
kwa wakati wote katika Vituo vya Afya kwani kunaweza kuwa na wataalam wakafanya
kila kitu lakini kama hakuna damu msaada hautofanya kitu chochote.
“Nawashukuru Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuona kuwa
kuchangia damu ni jambo la msingi, hali ya uhitaji wa damu ni kubwa hasa kwa
mikoa yenye idadi kubwa ya watu na tunatamani angalau kila mkoa uwe na asilimia
85 mpaka 90, tunaipongeza Timu ya Afya ya Mkoa wa Dodoma kwa kuvuka lengo
lililowekwa, nawasihi Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwa zoezi la uchangiaji
damu lisiwe kwenye Jukwaa hili tu bali muendelee kulifanya mara kwa mara kwani
damu lazima itolewe na wananchi wenyewe,” alisema Bi. Ziada.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
amewakaribisha wananchi kuchangia damu ili kuwa na damu ya kutosha katika ghala
za kutunzia damu kwa ajili ya kusaidia wenye uhitaji wakiwemo wagonjwa
waliopata ajali, wajawazito na watoto wenye upungufu wa damu.
Aidha, amesisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu hivyo, ambapo
kwa Mkoa wa Dodoma mahali pa kuchangia damu ni Kituo cha Damu Salama cha Kanda
ya Kati, Hospitali ya Mkoa wa Dodoma pamoja na Kituo cha Afya Makole.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali,
Bibi Mwantumu Mahiza amewashukuru wajumbe wa Mashirika hayo waliojumuika mkoani
Dodoma kwa ajili ya Jukwaa la Mwaka la Mashirika hayo. Pia amewashukuru kwa
kurudisha kwa jamii katika njia za kijamii zaidi ikiwemo kupanda miti takriban
300, kuchangia damu na kuona watoto yatima na wenye mazingira magumu.
“Kuchangia damu ni sadaka kubwa, hakuna kiwanda cha damu
wala biashara ya damu lakini unapotoa damu yako umetoa damu kwa ajili ya
kumsaidia mwanadamu mwenzio. Natoa wito kwa wajumbe wa mkutano wa mwaka huu na
wananchi wote ambao wana sifa za kuchangia damu waweze kufanya hivyo,” amemalizia
Mwenyekiti Mwantumu Mahiza.
Na Jacquiline Mrisho- MAELEZO
0 Maoni