Zaidi ya dola za Marekani bilioni 10 kuwekezwa katika biashara ya kaboni

 

Tanzania imepokea Makampuni zaidi ya 20 kutoka kwenye Mataifa mbalimbali Duniani ambayo yameingia mkataba wa kufanya uwekezaji katika Biashara ya hewa ya Kaboni unaotarajiwa kuwa wa thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani (USD) bilioni 10.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo alipokuwa akifunga Mdahalo wa Masuala ya Biashara ya Hewa ya Kaboni katika ukumbi wa Johari Rotana jijini Dar es Salaam.

“Mpaka sasa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi zake za Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) zimepokea makapuni zaidi ya 20 kutoka nchi za Kenya, Urusi, Singapore, Marekani, Kanada, Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Uswisi, Estonia, na Italia kuja kuwekeza katika biashara ya hewa ya kaboni” Mhe. Masanja amefafanua.

Amesema nchi hizo zimeshaingia makubaliano ya awali na Tanzania na baadhi ya mazungumzo yanaendelea kwenye taasisi husika chini ya usimamizi wa Kituo cha Uratibu wa Masuala ya Hewa ya Kaboni kilichopo Mkoani Morogoro (NCMC).

Mhe. Masanja ametaja maeneo yanayotarajiwa kuingia katika uwekezaji huo kuwa ni Misitu ya Hifadhi ya Serikali Kuu, Misitu ya Vijiji, Miradi ya Upandaji Miti, Hifadhi za Wanyamapori za Jamii, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Taifa.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufungua fursa ya biashara hiyo ya Kaboni, akihamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa hiyo.

Katika hatua nyingine Mhe. Masanja ameipongeza Kampuni ya Carbon Tanzania kwa kuwezesha baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Tanganyika ambavyo vimepata zaidi ya bilioni 8 kutokana na shughuli za maendeleo na uhifadhi.

Biashara ya Hewa ya Kaboni ni sehemu ya utekelezaji wa kifungu (article 6.2) cha Makubaliano ya Mkataba wa Paris unaolenga kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.

Chapisha Maoni

0 Maoni