Wahariri wahimizwa kuiendeleza lugha ya Kiswahili

 

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mh. Hemed Suleiman Abdullah, amewataka wahariri wakuu wa vyombo vya habari nchini kutekeleza majukumu ya kuilinda na kuiendeleza lugha adhimu ya Kiswahili.

Mh. Abdullah ametoa kauli hiyo Zanzibar katika semina ya Wahariri Wakuu wa Vyombo Vya Habari, iliyolenga namna bora ya kutumia Kiswahili Sanifu katika Vyombo Habari, katika kuelekea Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7.

Amesema kwamba vyombo vya habari vinamchango mkubwa katika kueneza lugha ya Kiswahili, kutokana kuwa na uwezo wa kuwafikia wananchi wengi, hivyo ni vyema vikaitumia vizuri lugha hiyo.

“Wengi wenu wanaitumia vizuri lugha ya Kiswahili, ila wapo wachache wanao kiharibu Kiswahili, ama kwa kutokujua au kwa kutia mbwembwe,” amesema Mh. Abulallah.

Aidha, Mh. Abdullah amewataka wahariri, kutumia fursa zilizopo katika vyombo mbalimbali vya habari vya Kimataifa ili kukikuza Kiswahili sanifu katika ngazi ya kimataifa.

Kwa upande wao Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Zanzibar Mh. Tabia Mohamed Mwita na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo (Bara) Mh. KHamis Mwinyijuma walielezea mikakati mbalimbali inayofanywa katika kukuza Kiswahili.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji China, (CMG) Nairobi Bi. Du Shungfang alitoa wito wa kuandwa kwa umoja wa vyombo vya habari vinavyotumia lugha ya Kiswahili, ili kuendelea na kuikuza lugha hiyo.

Pia Bi. Du ametaka kusimamiwa ipasavyo mitandao inayofasiri lugha ya Kiswahili kama ya google ambayo imekuwa na makosa ya kisanifu na kupotosha watu wanayoitumia ili kufahamu Kiswahili.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Kiswahili Duniani, iliyoanza kuadhimishwa rasmi tangu mwaka 1922, kwa maagizo la UNESCO ni “Kiswahili Chetu, Umoja Wetu”.

Chapisha Maoni

0 Maoni