Afrika kushuhudia uzinduzi jezi mpya ya Simba kilele cha Mlima Kilimanjaro

 

Klabu ya Simba imedhamiria kuionyesha Afrika uzinduzi wa jezi mpya itakayotumiwa katika msimu wa mwaka 2023/2024 tukio hilo ambalo litafanyika katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro almaarufu Paa la Afrika.

Zoezi linalotegemea kufanyika Julai, 21 katika kilele cha Mlima Kilimanjaro chenye urefu wa mita 5895 kutoka usawa wa bahari.

Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wapanda Mlima hao kupeleka jezi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Abdallah Mwaipaya aliipongeza Klabu ya Simba kwa ubunifu huu na uzalendo wa kuitangaza nchi yao.

“Hili ni tukio kubwa ambalo Klabu ya Simba wamelifanya kuuongezea thamani Mlima Kilimanjaro na utalii kwa ujumla kwa nchi yetu, niwatake mashabiki wote wa Simba waliopo katika mikoa ya jirani na Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi kuwapokea wapandaji Mlima wanaporejea siku ya jumamosi” alisema Mhe.Mwaipaya.

Naye, Msemaji wa Simba SC Ahmed Ally alisema “Jezi zetu zitazinduliwa Julai, 21 2023 Juu ya Kilele cha Mlima Kilimanjaro saa 1:00 Usiku tukio litakalokuwa Mubashara kutoka Mlimani” Amesisitisa Ahmed Ally.

Pia, Ahmed Ally alielezea sababu za jezi ya Simba SC kuzinduliwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro ni kutokana na maono ya kuiunga mkono serikali kwenye suala zima la kutangaza na kukuza utalii wa ndani.

“Nyote mnafahamu kwa muda wa miaka mitano sasa tumekuwa tukitumia utambulisho wa ‘VISIT TANZANIA’ katika jezi zetu na katika jezi ya msimu uliopita ilikuwa na alama ya Mlima Kilimanjaro hii ni ishara kwamba Simba tupo bega kwa bega na Serikali kupigania utalii wa nchi yetu” alisema Ahmed Ally.

Vile vile, Ahmed Ally alisema kuweka nembo za mlima huo katika jezi zetu tuliona haitoshi na kuamua ni lazima Afrika na Dunia nzima kuona jezi hiyo na kutambulisha utalii na Mlima wetu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro Afisa Uhifadhi Mkuu, Mapinduzi Mdesa alitoa rai kwa klabu nyingine nchini kuiga mfano wa Klabu ya Simba nakuja na mawazo mengine ya kutangaza utalii wetu.

“Huu ni ubunifu ambao Klabu ya Simba imekuja nao kama Hifadhi tunachukulia ni jambo zuri sana katika kutangaza utalii wa ndani hivyo kupitia zoezi hili tunaimani kwamba inaenda kuhamasisha watanzania wengi lakini pia waafrika na watu wote duniani kuvutiwa kupanda Mlima Kilimanjaro, nitoe wito kwa klabu zingine kuja na ubunifu wao kupitia maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kuja kufanya hamasa kwa mashabiki wao na kwa watanzania kwa ujumla”.

Na. Edmund Salaho- Kilimanjaro

Chapisha Maoni

0 Maoni