Kampuni zisizosajili wamiliki manufaa zaiweka nchi matatani

Kampuni 20,000 tu, kati ya kampuni 80,000 nchini ndio zimewasilisha majina ya wamiliki manufaa kwa kuzingatia mabadiliko ya sheria ya kampuni iliyotambulisha dhana mpya ya Umiliki Manufaa, inayohimiza uwazi na uwajibikaji.

Dhana hiyo mpya imeanza kutumika rasmi baada ya kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ya kampuni sura namba 212 ya mwaka 2022, na Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuidhinisha kanuni zake kuanza kutumika.

Akiongea kwenye warsha ya Wahariri kuhusu dhana ya Umiliki Manufaa, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Makampuni na Majina ya Biashara wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Meinrad Rweyemamu amezitaka kampuni kusajili wamiliki manufaa.

Amesema kwamba jambo la kuwasilisha majina ya wamiliki manufaa ni la kulipa kipaumbele, kutokana na kuwa ni takwa la kimataifa na Tanzania inafanyabishara duniani hivyo lisipotekelezwa nchi itafungiwa kufanya biashara.

"Kwa sasa tupo katika 'Grey list' (orodha ya kijivu) hii si nzuri kwa taifa kwani tupo karibu na 'danger zone' (eneo hatari), tunaweza tukajikuta tunafungiwa kufanya biashara duniani," alisema Bw. Rweyemamu.

Amesema kuwa lengo la dhana ya Umiliki Manufaa, linajikita katika kudhibiti vitendo vya utakatishaji fedha, pamoja na kampuni ambazo zilizuliwa kufanya kazi kutokana na wamiliki wake kujihusisha na uhalifu.

Bw. Rweyemamu amesema kwamba ni kosa kwa kampuni kutotoa taarifa za wamiliki manufaa ama kutoa taarifa za uongo kuhusiana na wamiliki hao, ambapo faini yake ni kuanzia shilingi 5,000,000 hadi shilingi 10,000,000.

Akifafanua kuhusu ni nani haswa ni mmiliki manufaa, Bw. Rweyemamu amesema kuwa ni lazima awe ni mtu na awe ndio mtu ambaye ni mmiliki mkuu wa mwisho, ambapo kwa sasa kampuni nyingi nchini zinasajiliwa lakini mmiliki halali haonekani.

Pamoja na mambo mengine, Bw. Rweyemamu amesema kwamba kwa sasa nchini si lazima kwa BRELA kutoa taarifa za wamiliki manufaa kwa umma, ila kwa baadae huenda ikaruhusiwa ili itakuwa ni kwa kutoa malipo.

Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ndiye aliyefungua warsha hiyo ya siku moja kuhusu ‘Umiliki Manufaa’ iliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa  Biashara na  Leseni (BRELA), Dar es Salaam.

Chapisha Maoni

0 Maoni