Leseni za udereva 3,214 C,E zafutwa


Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani limezifuta leseni 3,214 za madaraja C na E za madereva waliokuwa wakiendesha malori na mabasi ya abiria.


Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’anzi akizungumza na mwandishi wa gazeti la Habari leo amesema  kuwa leseni zilizofutwa ni kati ya leseni 20,940 zilizohakikiwa hadi Aprili 30, mwaka huu.


Kamanda Ng’anzi alitaja sababu za kufutwa leseni hizo ni pamoja madereva waliokuwa wakimiliki leseni hizo kutokuwa na  sifa ikiwamo ya kusomea madaraja hayo.


Alisema leseni zilizofutwa zilionekana kutokidhi vigezo kwa sababu wahusika wamezipata visivyo halali na wameshushwa madaraja hadi ya awali ambayo ni D na B.



Kamanda Ng’anzi alisema leseni 17,726 zilibainika kuwa zimekidhi vigezo na hadi sasa wamehakiki asilimia mbili ya leseni za madereva wa madaraja C na E.


ZOEZI LA UHAKIKI

Akifafanua kuhusu uhakiki huo alisema  awamu ya kwanza ulianza Machi Mosi kwa hiari kwa madereva kutakiwa kufika ofisi za wakuu wa usalama barabarani kuhakiki leseni zao na kazi hiyo ilipangwa kukamilika Aprili 30, mwaka huu.


Kamanda Ng’anzi alisema wameongeza muda hadi Julai 31, mwaka huu ili kutoa nafasi kwa madereva kusomea madaraja E na C kwa sababu kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu za jeshi, ni lazima dereva apite katika shule za udereva.

“Niliwaambia wakuu wa usalama barabarani madereva wasibuguziwe tuwaache wenyewe waje kwa hiyari ila tukianza kuwapekuwa na kuwakamata tutawauliza na kuwahoji katika kipindi hiki tulichokuwa tumetoa muda wa kuhakiki wa hiyari walikuwa wapi kuhakiki,” alisema Kamanda Ng’anzi.


ULIPOANZIA 

Februari 2023 Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali Camilius Wambura alilifuta Dawati la Leseni la Jeshi la Polisi baada ya kubaini kuna ukiukwaji wa maadili.

Baada ya uamuzi huo, liliundwa dawati jipya la utoaji wa leseni na kikosi kilitakiwa kuhakiki ni leseni zipi zilipatikana kiuhalali na zipi hazikufuata utaratibu na kujua dereva gani ni mahiri katika eneo lake la kazi.

Chanzo:Habarileo

Chapisha Maoni

0 Maoni