SERIKALI imesema Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano unalenga kufikisha Pato la Taifa takribani shilingi trilioni 313 (Dola za Marekani bilioni 118.052) ifikapo mwaka 2030/31.
Akieleza kuhusu mpango huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk. Tausi Kida amesema mpango huo wenye kaulimbiu ya ‘Mageuzi kwa Ajili ya Ukuaji Jumuishi wa Uchumi na Uzalizaji wa Ajira’ una shabaha kuu sita ikiwemo kuongeza mchango wa sekta ya viwanda hadi asilimia 30 ya Pato la Taifa na kuzalisha zaidi ya megawati 8,000 za umeme.
Shabaha nyingine zinajumuisha kupanua upatikanaji wa huduma za intaneti kwa wananchi wote, kuzalisha ajira mpya zenye staha milioni 8.5, na kupunguza umaskini uliokithiri kitaifa kuwa chini ya asilimia tano huku kipaumbele kikiwekwa katika kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda, kuimarisha sekta binafsi, kuboresha mazingira ya biashara, na kuendeleza usimamizi mzuri wa miji, ardhi na mazingira.
Akizungumzia mpango huo, Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa ni nyenzo ya kimkakati inayolenga kujenga msingi wa taifa lenye ustawi, huku akisisitiza kuwa shabaha kuu ni kufikia uchumi wa Dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050 na kwamba kila Mtanzania, taasisi za umma, sekta binafsi na washirika wa maendeleo wanapaswa kushirikiana katika kuleta mageuzi haya.
Ili kufanikisha malengo hayo, Mpango IV unalenga kuvutia rasilimali takribani shilingi trilioni 477.7 (Dola za Marekani bilioni 183) ambapo sekta binafsi imepangiwa kuchangia asilimia 70 kupitia njia mseto ikiwemo uwekezaji wa moja kwa moja, ubia kati ya sekta za umma na binafsi, masoko ya mitaji, fedha za tabianchi, na kuimarisha ufanisi wa mashirika ya umma yenye mali zinazozidi shilingi trilioni 92.3.

0 Maoni