Tanzania, IOM Kuimarisha Ushirikiano Kwenye Ajira na Uhamaji Salama

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) ili kutumia uhamaji kama kichocheo cha maendeleo, uwekezaji na fursa salama za ajira, akibainisha hayo alipokutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Amy Pope, katika Ikulu ndogo Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walijadili namna bora ya kuoanisha vipaumbele vya IOM na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika maeneo ya ajira, diaspora, uwekezaji, usimamizi wa mipaka, afya, pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia wakati wa dharura za kibinadamu ili kulinda mazingira na afya za wanawake.

Rais Samia alisisitiza kuwa nchi ipo tayari kutumia ujuzi na mitandao ya diaspora kuharakisha maendeleo kupitia uwekezaji wa Watanzania wanaoishi nje, huku akieleza kuwa ushirikiano huo utaimarisha mifumo ya ajira za nje zenye staha na mikataba yenye maslahi, pamoja na kudhibiti uhamaji usio wa kawaida kwa kuzingatia misingi ya sheria na utu.

Kwa upande wake, Pope alisema IOM iko tayari kuisaidia Tanzania kuwaunganisha vijana na fursa halali za ajira duniani, mafunzo ya ujuzi, na kuimarisha mifumo ya uwekezaji na usimamizi wa mipaka, huku akitahadharisha vijana dhidi ya mitandao inayowalaghai kwa ahadi za uongo za ajira nje ya bara hilo.



Chapisha Maoni

0 Maoni