Umoja, amani
na mshikamano wa Tanzania unazidi kuimarika kupitia misingi thabiti ya utawala
wa sheria na utetezi wa maslahi ya wananchi, nguvu inayochagizwa na ushirikiano
wa dhati kati ya viongozi wa nchi, nguvu ya umma, na weledi wa wataalamu wa
sheria.
Akifungua
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali mnamo Julai 13, 2026,
katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa chama hicho
kinapaswa kuwa nguzo kuu ya kulinda utulivu wa nchi na si chanzo cha migongano
wala migawanyiko.
Rais alisema
kuwa Watanzania wana matarajio makubwa kutoka kwa mawakili na kuwataka
kutekeleze majukumu yao kwa uzalendo wa hali ya juu, uadilifu, na kulinda
maslahi ya taifa dhidi ya nguvu mbalimbali za kimataifa zinazotafuta kutimiza
ajenda zao binafsi kupitia mataifa mengine.
Katika
kuonyesha umuhimu wa kuzuia migogoro kabla haijatokea, Rais Samia amebainisha
kuwa kalamu ya Mwanasheria wa Serikali ni nyenzo yenye nguvu kubwa inayoweza
kuokoa rasilimali za umma na kuzuia hasara kubwa kwa serikali kabla hazijafika,
tofauti na kalamu ya Rais inayohusika katika hatua za mwisho za utekelezaji.
Ili
kuhakikisha kalamu hizo zinalinda rasilimali na uhuru wa nchi, serikali
imejijipanga kuendelea kuwajengea mawakili uwezo wa kitaaluma na kuboresha
mazingira yao ya kazi, ambapo Rais amemwagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.
Juma Homera, kutatua changamoto zao zikiwemo zile zilizofunguliwa njia tayari
kama upatikanaji wa ofisi na viwanja katika miji ya Dodoma na Arusha.
Amesema
mazingira wezeshi yatawezesha sekta ya sheria kuwa chombo chenye nidhamu,
maadili, na ubunifu kwa maslahi ya nchi.
Rais
alisisitiza kuwa nguvu ya kisheria inaenda sambamba na jitihada za kuwafikia
wananchi moja kwa moja ili kuwapa uwezo wa kujua haki zao, jambo ambalo
mawakili wa serikali wamekuwa wakilifanya kupitia kliniki za sheria na utafsiri
wa sheria mbalimbali kwenda kwenye lugha ya Kiswahili ili kukuza utawala wa
sheria kuanzia ngazi ya chini.
'Hatua hizi
ni sehemu ya maandalizi ya kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya
Taifa 2050, inayolenga kujenga sheria bora, mikataba imara, na taasisi
zinazowajibika ili kuvutia uwekezaji na kuchangia ukuaji wa uchumi shindani na
jumuishi. Kupitia mifumo hii, taifa linasimamia maendeleo ya kweli
yanayohakikisha kuwa hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika upatikanaji wa
haki na fursa za kimaendeleo'.
Hali
kadhalika, Rais Samia amesimama imara kuitetea taswira ya nchi kimataifa kwa
kuweka wazi kuwa Tanzania ni mfuasi makini na mzuri sana wa haki za binadamu
kupitia mifumo imara ya kisheria na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa.
Amekemea kwa
nguvu zote wimbi la sasa linalojaribu kuwaaminisha vijana kuwa serikali za
Afrika, hususan ya Tanzania, zinakiuka au hazifuati misingi ya haki za
binadamu, akisisitiza kuwa upotoshaji huo hauna nafasi katika taifa linalojali
utu na uwajibikaji.
Rais Samia ametoa wito kwa mawakili wote kuhakikisha kuwa taaluma yao haitumiwi kamwe kuhalalisha ajenda zenye nia ovu dhidi ya taifa, bali iendelee kuwa ngao ya kulinda uhuru, amani, na utu wa kila Mtanzania.


0 Maoni