Waziri Katambi awataka vijana kulinda amani

 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amewataka vijana nchini kuipenda nchi yao, kulinda amani na kuendelea kuwa wazalendo ili kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Katambi ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana uliofanyika katika Chuo cha Mipango mkoani Dodoma. Amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa vijana kupitia kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana, hatua inayolenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili pamoja na kuwawezesha kiuchumi.

“Vijana ni nguvu kazi ya taifa, hivyo wanapaswa kuipenda nchi yao, kulinda amani na kutumia fursa zilizopo ili kuchangia maendeleo ya Tanzania,” amesema Katambi.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo utoaji wa mikopo kwa vijana ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuboresha maisha yao. Amewahimiza vijana kuchangamkia fursa hizo kwa manufaa yao binafsi na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwaunganisha vijana kupitia majukwaa mbalimbali ya majadiliano na ushiriki katika maendeleo.

“Ofisi yangu itaendelea kutumia majukwaa haya kusikiliza maoni ya vijana na kushughulikia kero zao kwa wakati ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na taifa,” amesema Shekimweri.

Katika kongamano hilo, vijana walipatiwa elimu kuhusu namna ya kutoa maoni yao katika maboresho ya dodoso la Baraza la Vijana, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana toleo la mwaka 2024, elimu ya uraia, uzalendo na kujitolea, pamoja na fursa za kiuchumi zinazopatikana katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na nchini kwa ujumla.

Chapisha Maoni

0 Maoni