Jamii mkoani Morogoro imetakiwa kuwa mstari wa mbele katika
kulinda maadili ya Taifa na kudumisha amani, huku wazazi wakionywa kutowaacha
watoto wao pekee katika wimbi la ukuaji wa teknolojia ya mitandao ya kijamii.
Akizungumza na wananchi, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa
Morogoro, Mhe. Sheilla Lukuba, amewataka wazazi kuziba pengo lililopo kati yao
na watoto wao katika usimamizi wa matumizi ya mitandao ili kuepuka madhara
yanayoweza kujitokeza.
“Nawaomba wazazi tusiache pengo kubwa kwa watoto wetu
kwenye suala hili la mitandao. Tumeshaanza kuona madhara yake, hivyo tuendelee
kuwasaidia watoto kwa kuwaongoza ili Taifa letu lisitoke kwenye utamaduni ambao
babu zetu walituachia,utamaduni wa amani na heshima kwa wakubwa,” alisema Mhe.
Lukuba.
Fursa za Kiuchumi kwa Vijana
Kwa upande wake, kijana na fundi ujenzi kutoka Mzumbe, Nuhu
Ally, ametoa rai kwa vijana wenzake kuacha kutumia mitandao kama sehemu ya
kuchochea vurugu, badala yake waitumie kama daraja la kujikwamua kimaisha.
Alisema mitandao hiyo ikitumika kwa heshima itawezesha
kujikwamua kiuchumi kupitia fursa za kibiashara zinazopatikana mtandaoni.
Aidha amewataka vijana wenzake kujiepusha na kuhamasishana
mambo yanayoweza kuchochea uvunjifu wa amani nchini.
Kulinda Tunu ya Amani
Naye Mwenyekiti wa Shirika la Kukuza Mila na Desturi Mkoa
wa Morogoro (SHIWAMILA), Ramadhan Divunyagale, amesisitiza umuhimu wa kila
Mtanzania kuithamini amani iliyopo na kuliombea Taifa pamoja na viongozi wake.
“Nchi yetu ni nchi ya amani, hivyo Watanzania wote wakiwemo
vijana tuendelee kulienzi Taifa letu kwa kudumisha amani na umoja. Tuendelee
kumwombea Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan na serikali yake ili ituongoze
vyema,” alieleza Divunyagale.
Wito huo wa wadau umekuja wakati ambapo mmomonyoko wa
maadili na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao yamekuwa yakitajwa kama
changamoto inayohitaji nguvu ya pamoja kati ya serikali, viongozi wa kijamii,
na wazazi kuanzia ngazi ya familia.

0 Maoni