Ushindi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)
nchini Eswatini si tukio la bahati, bali ni matokeo ya ujasiri wa Serikali
kuachana na mifumo ya kizamani na kukumbatia teknolojia kama nyenzo ya
kurejesha heshima ya mkulima.
Tukio hili linathibitisha kuwa Tanzania sasa imeamua
kutumia akili ya kitafiti na uweledi wa hali ya juu wa wataalamu wake wa ndani
kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Ufanisi huu umewezekana kutokana na usimamizi madhubuti wa
Wizara ya Kilimo ambayo iliamua kuweka msukumo katika mifumo inayoziba mianya
ya upotevu.
Serikali imekuwa ikisimamia kwa karibu uundaji wa Mfumo wa
Kidijiti wa Pembejeo za Ruzuku, ikilenga kuhakikisha kuwa kila shilingi
inayowekezwa kwenye kilimo inamfikia mlengwa halisi ambaye ni mkulima . Hatua
hii imepunguza kwa kiasi kikubwa urasimu na udanganyifu uliokuwa ukijitokeza
katika ugawaji wa mbolea nchini.
Kiwango cha utaalamu kilichoonyeshwa na TFRA katika
mashindano hayo yaliyoshirikisha taasisi nyingi barani Afrika, ni uthibitisho
kuwa vijana wa Kitanzania wana uwezo wa kubuni mifumo ya kidijiti inayoweza
kushindana kimataifa.
Wataalamu wa TEHAMA ndani ya mamlaka hiyo wameonyesha uwezo
mkubwa wa kutengeneza mifumo inayozungumza na mahitaji ya nchi, jambo ambalo
limefanya mataifa mengine makubwa kama Afrika Kusini kutambua uwezo wa
Tanzania.
Maana yake ni kwamba Tanzania sasa inakuwa kitovu cha
maarifa ya teknolojia ya kilimo barani Afrika, ambapo nchi nyingine zinaanza
kugeuza macho huku ili kujifunza siri ya mafanikio haya.
Kwa mkulima wa Tanzania, mafanikio haya yana tafsiri ya
moja kwa moja kwenye maisha yake ya kila siku. Mfumo huu wa kidijiti unampa
mkulima uhakika wa kupata pembejeo kwa wakati na kwa bei elekezi, bila
kuingiliwa na watu wa kati wasio waaminifu.
Hii ina maana kuwa ruzuku ya serikali sasa inafanya kazi
iliyokusudiwa, ambayo ni kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija
shambani. Matokeo yake ni ongezeko la mavuno yanayopelekea usalama wa chakula
na kuinua uchumi wa kaya za wakulima nchi nzima.
Ushindi huu pia ni ujumbe mzito kwa taasisi nyingine za
umma. Kwa kuwa mfumo huu sasa umeanza kutumiwa na taasisi kama TOSCI, COPRA, na
Bodi ya Korosho, ni wazi kuwa Tanzania inaelekea kwenye mfumo mmoja jumuishi wa
kidijiti utakaorahisisha huduma zote za kilimo.
Hii ndiyo maana halisi ya maendeleo; kutumia teknolojia
kurahisisha maisha ya watu na kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa na
kutumika kwa manufaa ya wengi, huku tukiandika historia mpya barani Afrika kama
taifa la wabunifu na wazalishaji.

0 Maoni