Ziara ya
wataalamu wa misitu kutoka Jimbo la Hunan, nchini China, imeingia hatua ya pili
baada ya ujumbe huo kutembelea Makao Makuu ya Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) yaliyopo Itega, Dodoma. Lengo la ziara hiyo ni kuweka msingi wa
ushirikiano wa muda mrefu katika masuala ya uhifadhi, utafiti na utalii wa
kiikolojia kati ya taasisi hizo mbili.
Mazungumzo
yaliyofanyika jana yalihitimishwa kwa makubaliano ya awali ya kuandaa
makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya TFS na Idara ya Misitu ya Hunan.
Makubaliano hayo yataainisha maeneo mahsusi ya ushirikiano, yakiwemo tafiti za
pamoja, ubadilishanaji wa wataalamu na kukuza utalii wa mazingira asilia,
hususan katika hifadhi za misitu.
Akizungumza
baada ya kikao hicho, Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu, Prof. Dos Santos Silayo,
alisema makubaliano hayo yatatoa dira mpya ya ushirikiano wa kimataifa katika
kulinda misitu, kukuza tafiti za pamoja na kuendeleza utalii unaohusisha jamii
katika shughuli za uhifadhi.
“Tumeafikiana
kuandaa mfumo wa ushirikiano wa muda mrefu utakaowezesha kubadilishana
wataalamu, teknolojia za uhifadhi, na kukuza tafiti za pamoja za utalii wa
kiikolojia. Hii ni fursa kubwa ya kuimarisha diplomasia ya uhifadhi na kulinda
misitu yetu kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” alisema Prof. Silayo.
Kwa upande
wake, Kiongozi wa Ujumbe wa Wachina ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu
ya Hunan, Jianga Rui, alisema Serikali ya China imeweka dhamira ya kuanzisha
uhusiano wa kindugu kati ya hifadhi za misitu za nchi hizo mbili. Alisema
dhamira hiyo inalenga kuimarisha uelewa wa pamoja kuhusu uhifadhi wa mazingira
na maendeleo ya utalii wa misitu.
“Tumevutiwa
na mfumo wa Tanzania wa usimamizi wa hifadhi na namna jamii inavyoshirikishwa
katika uhifadhi. Tunataka kujifunza kutoka kwenu na kuanzisha miradi ya pamoja
itakayokuza uhusiano wa kirafiki na kukuza utalii wa mazingira asilia,” alisema
Jianga Rui.
Aliongeza
kuwa, kwa mujibu wa taratibu za ndani za mkoa wa Hunan, ushirikiano huo
utapitia njia za kidiplomasia. Hivyo, baada ya kurejea China, timu yake
itawasilisha taarifa rasmi kwa mamlaka husika ili kuratibu maandalizi ya rasimu
ya makubaliano hayo.
“Tutawasilisha
ripoti kwa mamlaka yetu na baada ya kupata idhini, tutaandaa rasimu ya
makubaliano ya ushirikiano. Tutadumisha mawasiliano ya karibu ili kuhakikisha tunasonga
mbele katika utekelezaji wake,” alisema.
Mazungumzo
hayo ni mwendelezo wa ziara ya siku nne ya ujumbe huo, uliotembelea awali
Hifadhi za Mazingira Asilia za Pugu–Kazimzumbwi mkoani Pwani, ambako walijionea
namna TFS inavyotekeleza uhifadhi shirikishi unaowezesha jamii kunufaika
kupitia utalii wa kiikolojia.
“Mfumo wa
TFS unatoa somo kwa dunia kuhusu jinsi uhifadhi na maendeleo ya jamii
vinavyoweza kwenda sambamba,” aliongeza Jianga Rui.



0 Maoni