Ikiwa
zimesalia siku chache kuelekea kufunga mwaka wa 2025, Bustani ya Wanyamapori
Hai Tabora, maarufu Tabora Zoo, Hifadhi inayotajwa kubeba historia iliyopea Kwa
vipeo inaendelea kuwa kivutio cha makundi mbalimbali ya watalii wanaofika kwa
ajili ya shughuli za utalii, mafunzo na kubarizi.
Mnamo
Novemba 8, 2025, Umoja wa Akina Mama Mahiri (MMN) kutoka Wilaya ya Sikonge
ulifanya ziara maalum katika bustani hiyo ili kujionea vivutio vya kipekee vya
utalii vinavyopatikana ndani yake ikiwemo mandhari ya asili pamoja na wanyamapori
hai kama tembo, nyumbu, hasa "nyumbu mwongozo wa watalii", ngiri
maarufu “Kasongo”, simba, chui na duma, sambamba na spishi mbalimbali za ndege
nyuni wakiwemo tausi na kasuku mapenzi, wanaopamba anga la Mkoa wa Tabora kwa sauti na rangi zao za kuvutia.
Kwa kipindi
cha hivi karibuni, Tabora Zoo imejipatia umaarufu mkubwa na kuwa kimbilio la
watalii wengi kutoka ndani na nje ya mkoa huo. Hii ni kutokana na ongezeko la
wanyamapori hai pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya utalii uliofanywa na
Serikali kupitia TAWA, ikiwemo eneo la michezo ya watoto linaloongeza burudani
na furaha kwa familia na wageni wanaotembelea bustani hiyo.
Aidha, TAWA
inaendelea kuwakaribisha wananchi wote kutembelea hifadhi hiyo, ikiwemo taasisi
za serikali, taasisi binafsi, vikundi vya vikoba, vyama na mashirika
mbalimbali, kwa ajili ya vikao, mafunzo, sherehe za harusi na shughuli nyingine
za kijamii zinazoambatana na utalii.




0 Maoni