Mahenge, eneo lililopo mkoani Morogoro, Wilaya ya Ulanga limeendelea kujipatia umaarufu mkubwa duniani kutokana na madini adimu ya vito aina spineli, hali ambayo sasa inaliweka eneo hilo katika ramani ya utalii wa madini nchini Tanzania.
Hayo
yalibainishwa Novemba 10, 2025 na
Mhandisi Penina Mtego ambaye ni
msimamizi mgodi wa Ruby International
unaosimamia uchimbaji wa madini ya spineli katika kijiji cha Epanko.
Mhandisi
Penina alielezea sababu iliyopelekea
kuanzishwa kwa kituo cha Utalii wa madini ya Spineli ni kutokana na
ubora wa madini hayo ambapo yanapelekea
kuonekana kama yanatengenezwa maabara jambo linalopelekea wafanyabiashara
wa madini ya vito kimataifa, watafiti na
wadau mbalimbali kufika mahenge ili
kujionea sehemu halisi yanapochimbwa madini hayo ikiwa pamoja na kutembelea
sehemu maalum yanapohifadhiwa.
Mhandisi
Penina alifafanua kuwa, madini ya spineli kutoka Mahenge yanajulikana kwa uzuri
wake wa kipekee, hususan rangi yake ya waridi na nyekundu inayong’aa, ambayo
inavutia wanunuzi na wachimbaji wa vito kutoka mataifa mbalimbali.
Aliongeza
kuwa, Spineli ya Mahenge imekuwa ikitajwa mara kwa mara katika maonyesho ya
vito ya kimataifa kama Tucson Gem Show nchini Marekani , Hong Kong Jewellery
Fair na BangKok Thailand ikiifanya Tanzania kuwa miongoni mwa vyanzo muhimu vya
madini bora duniani.
Naye, Salehe
Mbura anayesimamia kitengo cha
uzalishaji katika mgodi huo alisema kuwa, uwepo wa madini hayo umekuwa
chachu ya kuibuka kwa aina mpya ya utalii unaoitwa utalii wa madini, ambapo
wageni hutembelea migodi, kujifunza kuhusu malezi ya madini, na kushuhudia
shughuli za uchimbaji wa kiasili. Wengine huja kwa ajili ya biashara, utafiti,
au kutembelea maeneo ya kihistoria yanayohusiana na uchimbaji wa madini hayo.
Mbura aliongeza
kuwa, pamoja na kuvutia wageni, utalii wa madini Mahenge umechangia kukuza
uchumi wa eneo hilo kwa kuleta fursa mpya za ajira katika sekta za malazi,
usafiri, uuzaji wa vito, na utamaduni. Wakazi wa vijiji jirani wamenufaika
kupitia mauzo ya bidhaa za ndani na huduma kwa wageni.
Kwa upande
wake Mhandisi Migodi kutoka Ofisi ya Madini Mkazi, Mkoa wa Kimadini Mahenge
Mhandisi Joseph Ng'itu alieleza kuwa, madini ya spinel yamekuwa si tu hazina ya
thamani kwa Tanzania, bali pia daraja la kuunganisha uchimbaji, biashara, elimu
na utalii. Kwa usimamizi endelevu, Mahenge inaweza kuwa kitovu cha utalii wa
madini barani Afrika, ikichangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, aliongeza
kuwa, katika kituo hicho eneo lingine
linajumuisha makumbusho ya madini, maonesho ya vito, na mafunzo kwa
wachimbaji wadogo.




0 Maoni