Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya
Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wamepongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuchaguliwa kwake katika uchaguzi
uliofanyika Oktoba 2025.
Aidha wakuu hao pia waliwapongeza viongozi wengine
waliochaguliwa katika chaguzi zilizofanyika kati ya Septemba na Oktoba 2025
ambao ni Rais wa Malawi, Prof. Arthur Peter Mutharika, na Rais wa Seychelles,
Dkt. Patrick Herminie.
Pongezi hizo zimetolewa katika Mkutano Maalumu wa Wakuu wa Nchi na Serikali
(Extraordinary Summit) uliofanyika kwa njia ya mtandao Novemba 7, 2025, ambapo
viongozi hao walijadili masuala muhimu ya kikanda.
Pamoja na pongezi Mkutano huo wa SADC ulieleza masikitiko yake makubwa kwa matukio
ya vurugu katika nchi za Tanzania na Madagascar zilizosababisha kupotea kwa
maisha, pamoja na uharibifu wa mali za umma na miundombinu muhimu.
Katika mkutano huo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
iliwakilishwa na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ambaye
alisema kwamba kwa sasa hali ni shwari nchini Tanzania na kuwa serikali
inajipanga kwa mazungumzo kwa ajili ya kuleta mtangamano wa taifa.
Mkutano huo ulikubali uamuzi wa Jamhuri ya
Madagascar kuachia wajibu wake kama Mwenyekiti wa SADC kufuatia maendeleo ya
kisiasa yaliyoathiri uwezo wake wa kutekeleza majukumu ya nafasi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Jamhuri ya Afrika Kusini
ambayo ni naibu katika uongozi SADC kwa sasa imechukua nafasi ya uenyekiti hadi
Agosti 2026 kwa mujibu wa katiba ya jumuiya hiyo.
Mkutano huo pia ulikubaliana kuendelea kutekelezwa
kwa Kaulimbiu iliyopitishwa katika Mkutano wa 45 wa SADC uliofanyika
Antananarivo, Madagascar, mwezi Agosti 2025 isemayo "Kuendeleza Ukuaji wa Viwanda, Mabadiliko
ya Kilimo, na Mpito wa Nishati kwa SADC Imara" hadi Agosti 2026.
Mkutano Maalumu huu wa SADC ulifanyika kwa mwaliko
wa Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa.

0 Maoni