Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.
Hassan Abbasi, ameuaminisha ulimwengu kwamba hali ya utalii na amani nchini
Tanzania ni imara na waje watembee na kuwekeza.
Ametoa kauli hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa 26 wa
Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism), ulioanza Novemba 9, 2025, jijini Riyadh, Saudi Arabia,
kufuatia vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi katika baadhi ya
maeneo.
Alisema hayo akichangia Ripoti ya Mwaka ya
Utekelezaji ya shirika hilo, ambapo Tanzania pia ilinufaika na programu
mbalimbali, ikiwemo kuandaa Mkutano wa Kanda ya Afrika wa Utalii wa Chakula
(Gastronomy Tourism) uliofanyika Arusha mwezi Aprili, pamoja na ufadhili wa baadhi
ya programu za uhifadhi wa mazingira katika Milima ya Usambara.
“Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza hili, baada ya
kumpongeza Katibu Mkuu na Sekretarieti ya UN Tourism kwa utekelezaji ambao pia
Tanzania imenufaika nao, nitumie fursa hii kuripoti kwamba Tanzania iko salama
kufuatia tukio lililotokea wakati wa uchaguzi.
“Serikali imefanya jitihada na kurudisha nchi yetu
katika hali ya utulivu, na hivyo kuhakikisha inabaki salama kwa watalii, na
vivutio vyetu vyote, ambavyo mnajua, viko salama. Ninakaribisha wajumbe wa
Mkutano huu na wadau wengine wa utalii kuja na kuendelea kutembelea nchi hii,
ambayo ni kivutio bora zaidi Afrika kwa utalii wa safari,” alisema Dkt. Abbasi.
Aidha, mbali na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 32
tu kati ya wanachama 160 wa Shirika hilo, kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Utekelezaji (Executive Committee), Mkutano Mkuu huo pia uliidhinisha Tanzania
kuwa Mjumbe wa Kamati ya Hati za Utambulisho (Credentials Committee) ya UN
Tourism.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine, unajadili
matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) katika kukuza utalii.
Pia mkutano huo ulimthibitisha Sheikh Nasser Al Nowais kutoka UAE kama Katibu
Mtendaji mpya wa taasisi hiyo muhimu kwa sekta ya utalii duniani.



0 Maoni