Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa walimu ni nguzo kuu ya maendeleo ya taifa
lolote hapa duniani kwani ndio wanaotoa rasilimali watu yenye elimu ambayo ni
muhimu zaidi kwa Taifa.
Amesema
kuwa mafanikio ya kielimu, kijamii na kiuchumi yanatokana na juhudi za walimu
kwani walimu ni fahari ya familia, jamii na nchi na kupitia mikono yao vijana
wa kitanzania wanajengewa maarifa, stadi na maadili ya uzalendo.
Amesema
hayo Oktoba 03, 2025 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani ambayo
kiwilaya imeadhimishwa Bukombe mkoani Geita katika uwanja wa Shule ya Sekondari
ya Ushirombo.
"Kila
hatua ya ustawi wa kijamii na kiuchumi inaanzia darasani kupitia juhudi na
maarifa ya walimu. bila walimu, hakuna taaluma, hakuna viongozi wa kesho na
hakuna Taifa linaloweza kusimama imara, walimu ndio chimbuko la uvumbuzi na
ubunifu wa kizazi kipya."
Amesema
kuwa kwa kutambua umuhimu wa kada ya ualimu hapa nchini, Serikali ya Awamu ya
Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea
kuboresha mazingira ya kada hiyo ikiwemo kwa kupandisha madaraja na kuimarisha
mafunzo kwa walimu.
Ameongeza
kuwa ili kukabiliana na upungufu wa walimu nchini Serikali ya Awamu ya Sita
imeendelea kuthamini na kuwekeza katika kada ya ualimu kwa kuajiri walimu wapya
kila mwaka.
Kadhalika,
Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Ofisi ya Rais -
UTUMISHI kufanya msawazo wa walimu ndani ya mikoa husika kwa kuhakikisha kila
shule inapata walimu ili watoto wa Kitanzania wapate elimu bora.
"Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Vyuo vya Ualimu na Taasisi
ya Elimu Tanzania (TET) imarisheni mafunzo ya kitaaluma na endelevu kwa walimu
ili waendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya dunia ya leo".
Amesema Mhe. Majaliwa.
Naye,
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amesema kuwa taaluma ya
ualimu ndio taaluma pakee inayomtengeneza mtu awe bora kuliko hata ualimu
wenyewe na wakati wowote hujinyima muda wake na nguvu zake zote kumtengeneza
mtu kuwa mume au mke bora au hata mzazi bora.
"Taaluma
ya ualimu humfanya mtu kuwa raia mwema kwenye nchi na zaidi sana humfanya kuwa
mtumishi, mfanyakazi na mzalishaji mali bora, wakati wote wa maisha yake, hii
ni taaluma ambayo tunaamini ni ya uumbaji wa pili baada ya mwanadamu kuzaliwa
na wazazi wake, kazi ya pili huendelea hapa duniani na muumbaji huwa ni
mwalimu," amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza
kuwa Mwalimu ndiye anayetoa mwelekeo wa maisha ya kila mtu na ukiona jamii
yoyote yenye ustaarabu na kustaarabika huhitaji kupiga ramli kujua nani chanzo
chake bali mwalimu ndio sababu yake.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Caroline
Nombo amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya shughuli
mbalimbali zinazowawezesha walimu kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuleta
matokeo chanya ikiwemo ujenzi wa miundombinu shuleni na lengo ni kukuza
ujifunzaji na ufundishaji.
Ameongeza
“Serikali inathamini jitihada zinazofanywa na walimu kwani wamekuwa kiini cha
mafanikio. "Kila mmoja wetu amepita kwenye mikono ya walimu, tunawashukuru
walimu wote wanaotoa nguvu na maarifa yao kuwawezesha Watanzania."





0 Maoni