WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imeamua kuingiza mabasi 60 mapya
kwenye Barabara ya mabasi yaendayo haraka njia ya Kimara hadi Kivukoni
iliyokuwa na mabasi 30 yanayofanya kazi ili kukabiliana na upungufu wa magari
uliokuwepo.
Amesema kuwa
idadi hiyo itafanya njia hiyo kuwa na mabasi 90 ambayo kwa kiasi kikubwa
itasaidia kuondoa kero ya usafiri iliyokuwepo katika kipindi cha hivi karibuni.
Amesema
hayo leo Alhamisi (Oktoba 02, 2025) alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji
huduma ya usafiri kwa mabasi yaendayo haraka kwa njia ya Kivukoni hadi Kimara
jijini Dar es Salaam.
"Serikali
yenu baada ya kuruhusu makampuni binafsi tumeona tuchukue mabasi 60 kutoka
kampuni ya Mofat yaingie katika barabara hii na yameanza kutoa huduma leo, malengo
yetu ni kuondoa kadhia ya usafiri kwenye njia hii."
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza UDART na DART kuhakikisha wanasimamia matumizi ya kadi za kielektroniki katika utozaji wa nauli badala ya kutumia fedha taslimu (Cash) ili kudhibiti upotevu wa mapato katika usafiri huo.
"Na
tumeagiza kadi hizi zisiwe za mabasi haya pekeyake, tunataka zitumike kwenye
viwanja vya mipira, usafiri wa Azam marine, SGR, vituo vya mabasi, Mheshimiwa
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Jerry Silaa, tunataka
hili likamilike kwa haraka."
Pia,
Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Taasisi
ya Dart kuhakikisha wanasimamia
kikamilifu usafiri huo ili kupunguza kero ya usafiri wa mabasi hayo katika jiji
la Dar es Salaam.
Kadhalika,
Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kuiamini Serikali kwamba
itahakikisha kero ya usafiri katika njia hizo itapunguzwa kwa kiasi kikubwa ili
kuondoa tatizo la usafiri katika jiji la Dar es Salaam. "Haya
yaliyojitokeza tuamini sasa yamekwisha."
Akizungumzia
kuhusu maboresho hayo, Mmoja ya wasafiri amesema kuwa usafiri katika siku hiyo
umekuwa wa kuridhisha na wanasafiri kwa wakati “Kwasiku ya leo usafiri umekuwa
mzuri na magari yameingia kwa wakati.”


0 Maoni