Dkt. Mwinyi apiga kura, apongeza wananchi kudumisha amani

 

Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kufarijika na hali ya amani na utulivu iliyotawala katika vituo vya kupigia kura na nchini kwa ujumla.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 29 Oktoba 2025, baada ya kupiga kura katika Jimbo la Kwahani Kituo cha Kariakoo ndani, chumba no: 3, majira ya saa 2:25 asubuhi, akiambatana na Mkewe, Mama Mariam Mwinyi.

Mgombea huyo wa Chama Cha Mapinduzi amefahamisha kuwa kuwepo kwa hali ya utulivu kunatoa fursa pana kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kutimiza wajibu wao wa kikatiba na kidemokrasia.

Akielezea matumaini yake kuhusu Uchaguzi Mkuu huo, Dkt. Mwinyi amesema Chama Cha Mapinduzi kina matarajio makubwa ya ushindi kufuatia utekelezaji wa mafanikio ya Ilani yake ya 2020–2025 na miradi mikubwa ya kimaendeleo iliyotekelezwa katika nyanja mbalimbali.

Dkt. Mwinyi ameipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa maandalizi mazuri ya uchaguzi na kuwasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi wanaowataka.

Vyama 11 vya siasa vimesimamisha wagombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Chapisha Maoni

0 Maoni