Dkt. Samia awataka wanachama wa CCM kuvunja makundi

 

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho waliogombea nafasi mbalimbali kuvunja makundi na kuungana na walioteuliwa, ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika Septemba 5, 2025 katika Viwanja vya Sabasaba, mjini Njombe, Dkt. Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, aliwataka wanachama waliopitishwa na waliokosa uteuzi kuweka tofauti zao pembeni kwa maslahi ya chama.

“Nampongeza Mwenyekiti Deo Sanga kwa kauli yake thabiti ya kuvunja makundi. Huu ndiyo mwelekeo tunaoutaka. Makundi yote yavunjwe, sasa ni wakati wa mshikamano kwa ajili ya ushindi wa CCM kote nchini,” alisema Dkt. Samia.

Kauli hiyo imekuja baada ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga maarufu kama Jah People, kutoa wito kwa wagombea wote kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha ushindi wa chama kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani.

“Mwenyekiti, mimi tayari nimewaambia wagombea kwamba makundi nimeyavunja. Nimewaonya, mtu asije akaniambia fulani hakukubali au fulani hakupitishwa. Uchaguzi umekwisha, sasa kazi ni moja tu kutetea ushindi wa chama chetu,” alisema Sanga.

Sanga hakuteuliwa kuwania tena ubunge wa Jimbo la Makambako, nafasi iliyochukuliwa na Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Daniel Chongolo, lakini ameonyesha mfano wa kukubali maamuzi ya chama na kusisitiza mshikamano.

Vituo 50 vya Kuhifadhi Parachichi Kujengwa

Katika hatua nyingine, Dkt. Samia alitangaza mpango wa Serikali wa kuanzisha vituo 50 vya kuhifadhia zao la parachichi katika mikoa inayolima zao hilo kwa wingi, likiwemo eneo la Nyanda za Juu Kusini.

Alisema kati ya vituo hivyo, viwili vitajengwa katika Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, ili kuhakikisha zao hilo linaweza kuhifadhiwa wakati bei ya soko la dunia ikiwa juu, hivyo kuongeza kipato kwa wakulima.

“Tutaweka pia maofisa ugani maalum watakaoshughulikia zao la parachichi, hasa katika mikoa ya Njombe na Mbeya, kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya kitaalamu ya uzalishaji,” alieleza.

Serikali Kuwachukulia Hatua Wenye Mashamba ya Chai Wasiyoendeleza

Dkt. Samia aliwaonya wawekezaji waliomiliki mashamba makubwa ya chai ambayo hayaendelezwi, akisema Serikali haitasita kuyachukua. Alisisitiza kuwa wawekezaji hao watalazimika kulipa madeni wanayodaiwa na wakulima pamoja na wafanyakazi wao kabla ya mashamba hayo kuchukuliwa.

Msisitizo kwa Maendeleo ya Viwanda na Kilimo

Katika hotuba yake, Rais Samia pia alieleza dhamira ya Serikali kuendeleza mpango wa kuanzisha kongani za viwanda katika kila wilaya nchini, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo kwa kutoa ruzuku zaidi kwa wakulima. 

“Tunaendelea kuweka mazingira bora kwa ajili ya uzalishaji wa kilimo na viwanda. Hii ni sehemu ya mkakati wetu wa kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” alisema.

Kampeni Zaendelea Iringa

Baada ya mikutano hiyo ya Njombe, Dkt. Samia ameendelea na kampeni zake mkoani Iringa, ambako leo anatarajiwa kuhutubia wananchi katika maeneo ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Nyololo na Kalenga.

Na. Aboubakary Liongo - Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM

Chapisha Maoni

0 Maoni