Chama cha Wananchi (CUF) kimeahidi kuwa endapo kitapewa ridhaa ya kuongoza Serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kitahakikisha kila mtumishi wa umma nchini anajengewa nyumba ya kisasa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha maisha yao na kupambana na mizizi ya rushwa katika taasisi za umma.
Mgombea urais wa chama hicho, Gombo Samandito Gombo ametoa ahadi
hiyo Septemba 5, 2025, wakati wa mkutano
wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Malunga, Manispaa ya Kahama, mkoani
Shinyanga.
“Watumishi wa umma wengi wanapitia maisha magumu, hali
inayowasukuma kuomba au kupokea rushwa. Serikali ya CUF itakapoundwa, kila
mtumishi atajengewa nyumba ya kisasa. Tutaondoa njaa na shida, ili watoe huduma
kwa uadilifu,” alisema Gombo.
Msaada wa Kifedha kwa
Wazee kuanzia Miaka 60
Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa urais aliahidi kuwa
Serikali ya CUF itakapoundwa, itatoa fedha ya kujikimu kwa kila mzee mwenye
umri wa miaka 60 na kuendelea, bila kujali kama alikuwa mtumishi wa Serikali au
la.
“Hata kama mzee huyu hakufanya kazi serikalini, lakini aliitumikia nchi kupitia kilimo chake, uvuvi wake au ufugaji wake. Wote hao watajumuishwa kwenye mpango wa kupata pesa ya kujikimu kila mwezi. Rasilimali tulizonazo zinatosha kwa kila Mtanzania kuishi kwa furaha,” alisema.
0 Maoni