Mtu mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa katika ajali ya gari na pikipiki iliyotokea usiku wa kuamkia leo Septemba 26, 2025 katika eneo la Lalsela, Kata ya Samuye, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, mkoani Shinyanga.
Ajali
hiyo ilitokea majira ya saa 7:00 usiku na kuhusisha gari aina ya Toyota Kluger
lililokuwa likiendeshwa na Fabian Manoga (36), mkazi wa Tabora, ambalo
lilimgonga mwendesha pikipiki aina ya SUNLG, Sudi Dotto (20), ambaye alifariki
dunia papo hapo.
Taarifa
ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, imethibitisha kutokea kwa ajali hiyo
na kueleza kuwa pia kijana mwingine aliyefahamika kwa jina la Noel Paul (18),
mkazi wa eneo hilo, alijeruhiwa na anaendelea kupatiwa matibabu katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
“Ajali
hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva wa gari ambaye alikuwa akiendesha kwa
mwendo kasi na kuvuka upande usio sahihi wa barabara, kisha kugonga pikipiki
iliyokuwa mbele yake,” alisema Kamanda huyo.
Kwa
mujibu wa Kamanda huyo, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya
Manispaa ya Shinyanga, ukisubiri taratibu za mazishi.
Aidha,
Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa madereva na watumiaji wengine wa
barabara kuchukua tahadhari na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili
kuepusha ajali.
“Tunawakumbusha
madereva wote kuwa waangalifu, kufuata alama na sheria za usalama barabarani
wakati wote wanapotumia vyombo vya moto. Usalama wa maisha ya watu uko mikononi
mwao,” alisisitiza Kamanda huyo.
Ajali
hiyo imeacha simanzi kubwa kwa wakazi wa eneo la Lalsela, huku familia ya
marehemu ikieleza kupokea kwa huzuni taarifa za kifo cha kijana wao ambaye
alikuwa bado anajiandaa na maisha ya kujitegemea.

0 Maoni