Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Singida wamepongeza jitihada kubwa za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya madini, ikiwemo kugawiwa leseni na kuwekewa mazingira bora ya kufanya kazi zao kwa amani.
Pongezi hizo zimetolewa leo Agosti 23, 2025 wakati wa
Kongamano la Wachimbaji Wadogo wa Madini wa Mkoa wa Singida na Kanda ya Kati,
lililofanyika katika eneo la Sekenke One, Shelui – Wilaya ya Iramba, ambapo
mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde.
Wachimbaji hao wameleza kuwa, hatua ya Serikali kufuta na
kurudisha Serikalini leseni na maombi 2,648 ambayo hayakuwa yakifanyiwa kazi,
kisha kugawiwa upya kwa wachimbaji wadogo, imekuwa suluhisho la muda mrefu kwa
changamoto ya kuvamia maeneo na kuchimba bila leseni.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Waziri wa Madini Mhe.
Anthony Mavunde amesema mpango wa Serikali ni kuongeza kiwango cha utafiti wa
kina wa madini kutoka asilimia 16 kilichopo sasa hadi kufikia asilimia 50
ifikapo mwaka 2030, kupitia maono ya Vision 2030; Madini ni Maisha na Utajiri.
Amesema kuwa, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni
115 kwa ajili ya utafiti wa madini nchini, ikiwa ni pamoja na kununua helikopta
maalum yenye vifaa vya kisasa kwa ajili ya upigaji picha na utafiti wa anga,
sambamba na ujenzi wa maabara za kisasa za uchambuzi wa madini zitakazotumika
na wachimbaji wadogo.
Wakati huohuo, Waziri Mavunde amebainisha kuwa Kampuni kubwa
za madini zimeanza kujipanga kuwekeza katika Mgodi mkubwa wa dhahabu katika
Kanda ya Kati (katika mikoa ya Dodoma na Singida), hatua inayotarajiwa kuongeza
zaidi fursa za ajira, mapato ya Serikali na mchango wa sekta ya madini katika
uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji
Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), Bw. John Bina, alisema zaidi ya wachimbaji
wadogo milioni 6 wanashiriki kikamilifu katika shughuli za madini na
wamefanikisha sekta hiyo kuchangia hadi asilimia 40 ya mapato yote ya madini
nchini.
“Tunampongeza Rais Samia kwa maono yake ya kuendelea
kuithamini sekta ya wachimbaji wadogo. Hii ni heshima kubwa kwetu na ndiyo
maana leo tunasherehekea mafanikio haya,” alisema Bina.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, alisema
sekta ya madini ndiyo inayoongoza kwa kasi ya ukuaji kiuchumi ndani ya mkoa huo
na imewezesha Singida kuvuka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.
“Madini ndiyo injini ya uchumi wa Singida, na kwa sasa mchango mkubwa unatoka kwa wachimbaji wadogo waliowekewa mazingira bora ya kufanikisha kazi zao,” amesema.
Awali, akizungumza katika kongamano hilo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Sabai Nyansiri, amesema mkoa huo umefanikiwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali yatokanayo na sekta ya madini katika mwaka wa fedha 2024/25, baada ya kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 26 dhidi ya lengo la shilingi bilioni 24.
0 Maoni