Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi (INEC) imevihimiza vyombo vya habari nchini kuripoti kwa usahihi na
kwa wakati kuhusu taarifa zote zinazohusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili
kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.
Kauli hiyo imetolewa leo,
tarehe 1 Agosti 2025, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo,
Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, wakati wa ufunguzi wa
mkutano kati ya Tume na Wahariri wa Vyombo vya Habari.
Jaji Mwambegele amesema
vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu
ya mpiga kura na taarifa sahihi zinazowawezesha kufanya maamuzi ya msingi kwa
uhuru na kwa amani.
Aidha, amewasihi Wahariri
wa vyombo vya habari kutumia majukwaa yao kuwaelimisha na kuwahamasisha
wananchi waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza
kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu, utakayofanyika tarehe 29 Oktoba
2025.
Amesisitiza kuwa
ushirikiano kati ya Tume na vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika
kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na kwa kuzingatia sheria za uchaguzi.
Akitoa mada kuhusu
Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani
amesema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kufanikisha maandalizi
na uendeshaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Ameongeza kuwa, katika
nchi yoyote inayodhamiria kufanikisha jambo kubwa kama uchaguzi, vyombo vya
habari ndio msingi wa kwanza, kwani kupitia kwao, wananchi hupata taarifa
sahihi, zilizofanyiwa utafiti na kuhakikiwa.
Bw. Kailima amesema kuwa
bila ushirikiano wa karibu na vyombo vya habari, juhudi zote za Tume katika
kutoa elimu na taarifa kwa umma haziwezi kuwafikia walengwa.
"Maana yake kila
kinachotolewa na Tume hakiwezi kuwafikia wananchi iwapo vyombo vya habari
havitaamua jambo hilo lifanikiwe," amesema.
Ameongeza kuwa wadau wote
wa uchaguzi, vikiwemo vyama vya siasa, wanategemea vyombo vya habari kutoa
taarifa zitakazowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa
uchaguzi.
Amesisitiza kuwa vyombo
vya habari ndivyo vinavyoweza kuwa sauti ya kwanza ya kuonesha upotoshwaji wa
aina yoyote unaofanywa kwa bahati mbaya au kwa makusudi kuhusu Tume na kuhusu zoezi
la Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
“Tunawaomba na
kuwanasihi, kutumia nafasi na fursa mlizonazo kuhakikisha kunakuwepo na taarifa
za mara kwa mara za kuelezea kinachoendelea kuhusu uchaguzi,” amesisitiza
Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Aidha wahariri hao wamekumbushwa
kutumia kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ambayo ni “Kura Yako Haki
Yako Jitokeze Kupiga Kura” kwenye taarifa zao wanazozitoa kwa umma ikiwa ni
sehemu ya uhamasishaji kwa wananchi kujitokeza kupiga kura.
0 Maoni