Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa maendeleo katika sekta ya elimu
ndio mkombozi na mafanikio ya Taifa lolote duniani.
Amesema kwa kutambua hilo, uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
uliamua kuwekeza katika sekta hiyo ili kuhakikisha watoto wa kitanzania
wanapata elimu bora katika ngazi zote.
Amesema hayo wakati alipozungumza na wanafunzi na walimu wa shule ya
sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia iliyopo Ruangwa mkoani Lindi, wakati wa
hafla ya kuwapongeza wanafunzi wa kidato cha sita waliofanya vizuri katika
mitihani ya kitaifa iliyofanyika mwaka 2025.
“Mliopo shuleni na mnaokuja, tambueni kuwa tuna maeneo muhimu ya
kuwaelimisha, mtapata elimu iliyobora na imara itakayowapa maarufa na ujuzi ili
muweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.”
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya maboresho ya mitaala kwa
lengo la kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi yaliyopo duniani ikiwemo
mahitaji makubwa ya ajira kwa vijana.
“Mabadiliko haya yameifanya mitaala yetu itakayofundishwa shuleni kila
mwanafunzi akimaliza ana uwezo wa kutumia mazingira alimo na taaluma aliyonayo
kuyabadilisha kuwa uchumi.”
Akisoma matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka 2025, Makamu Mkuu wa Shule
Amon Chalamila hiyo amesema kuwa shule hiyo ilisajili wanafunzi 188 ambapo wote
walifanya mitihani na wanafunzi 90 walipata daraja la kwanza, wanafunzi 95
walipata daraja la pili, wanafunzi watatu walipata daraja la tatu na hakuna
mwanafunzi aliyepata daraja na nne na sifuri. “Ufaulu huu ni sawa
na GPA ya 2.34”.
0 Maoni