WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ametembelea Chuo Kikuu cha Kilimo cha Belarus (Belarusian State
Agrarian Technical University - BSATU) na kufanya mazungumzo na viongozi wa
chuo hicho wakiongozwa na Mkuu wa Chuo, Bw. Romaniuk Nikolai.
Mazungumzo hayo yamefanyika
leo (Jumatano, Julai 23, 2025) kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo hicho jijini
Minsk ambapo masuala ya ushirikiano baina ya vyuo vikuu vya Tanzania vikiwemo
vya Sokoine na DIT yalijadiliwa.
Waziri Mkuu aliwaeleza
viongozi wa chuo kikuu hicho jinsi Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilivyoboresha sera ya elimu ambayo inataka
elimu ya amali na stadi za ufundi ziwe sehemu muhimu katika mitaala ya mafunzo
yanayotolewa nchini kote.
Aliwaeleza viongozi hao
juu ya hati ya makubaliano kwenye sekta ya elimu iliyosainiwa jana mbele ya
Waziri Mkuu wa Belarus na kwamba sasa ni wakati muafaka wa kuangalia namna ya
kuandaa ziara za mafunzo, kubadilishana wanafunzi na wahadhiri ili kujengeana
uwezo kwa pande zote mbili.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Chuo Kikuu cha BSATU, Bw. Romaniuk Nikolai alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba
chuo hicho kipo tayari kuanza majadiliano na viongozi kutoka Wizara ya Elimu
ambao wamefuatana na Mheshimiwa Waziri Mkuu ili waone ni kwa namna gani
wanaweza kuanza kutekeleza mambo yaliyojadiliwa.
Alimweleza Waziri Mkuu
kwamba Chuo Kikuu hicho ambacho kilianzishwa mwaka 1954, kinaongoza nchini humo
kwa kutoa mafunzo kwenye fani za uhandisi, uchumi na utawala na kinashirikiana
na taasisi na mashirika rafiki 39 (affiliate organisations) yanayojihusisha na
masuala ya kilimo na uundaji wa mitambo ya kilimo na zana za kisasa.
Alisema wanalenga zaidi
fani za kitaalamu kwenye ufugaji wa wanyama na mitambo ya kilimo (animal
husbandry and agricultural mechanisation) ambapo asilimia 70 ya mafunzo
yanayotolewa chuoni hapo, hufanyika kwa vitendo (practicals) na kisha
mwanafunzi anapewa wiki 28 za kwenda nje ya chuo kufanya mafunzo kwa vitendo
(internship).
Mapema leo asubuhi,
Waziri Mkuu alikutana na Wawakilishi wa Muungano wa Kampuni za Belarus
zinazofanya biashara na mataifa ya Afrika (AFTRADE) kwenye ukumbi wa mikutano
wa hoteli ya President.
Katika ziara hiyo,
Mheshimiwa Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi,
Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Bw. Shariff Ali Sharriff, Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu, Naibu Katibu Mkuu Kilimo, Dkt.
Stephen Nindi na Balozi wa Tanzania nchini Urusi na Belarus, Balozi
Fredrick Kibuta.



0 Maoni