Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu
amewahimiza wananchi wilayani Karatu mkoani Arusha kuchangamkia fursa ya Mikopo
inayotolewa na Benki ya NMB ili kukuza biashara zao.
Dkt. Jingu ametoa wito
huo jana, wakati akihutubia mkutano wa kuwafahamisha fursa zinazotolewa na
Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Wilayani humo.
“Ujumbe wangu kwenu ni
kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Mhe.
Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na
Makundi Maalum, imeweka mazingira rafiki kwa wafanya biashara ndogondogo kupata
mikopo ya aina mbalimbali ili mueweze kuendesha shughuli zenu za kiuchumi kwa
maendeleo yenu na Taifa” amesema Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa
wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa ya kushindania fursa ya manunuzi ya
serikali ya asilimia 30 ambayo inatolewa na taasisi zote za Serikali.
Baada ya marekebisho ya
sheria ya ununuzi wa umma mwaka 2023, sasa wananchi mnaweza kujiunga katika
vikundi mkiwa na biashara au huduma fulani, mnaweza kupata tenda za Serikali
ambazo zinapatikana katika Halmashauri zote nchini.
Naye Katibu Tawala wa
Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Juma Hokonoro amesema kuna fursa mbalimbali za
kiuchumi zikiwemo za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayoendesha mafunzo ya
kilimo na ufugaji hivyo ni muhimu wananchi wakazichangamkia kwa lengo la
kuongeza kipato na kukuza uchumi wao.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Shirika Lisilo la Kiserikali la Food for His Children Honorina
Honorata amesema kupitia Shirika hilo wataendelea kutoa mafunzo ya ufugaji na
kilimo kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya kuwezesha jamii kuondokana na umaskini.
Na. WMJJWM- Karatu

0 Maoni