Mamia ya washiriki leo,
Julai 13, 2025, wamejitokeza kushiriki Nyuki Marathon ya pili iliyofanyika
kwenye viwanja vya New AICC jijini Arusha, ikiwa na lengo la kuhamasisha
ufugaji nyuki na kuonesha mchango wake katika uchumi wa mtu mmoja mmoja na
taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa
mbio hizo, Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),
Prof. Dos Santos Silayo, alisema Nyuki Marathon ni zaidi ya tukio la michezo
kwani inaleta ujumbe wa maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 50
wa Shirikisho la Kimataifa la Wafugaji Nyuki Duniani (Apimondia) mwaka 2027.
“Michezo kama hii inatupa
fursa ya kuwaleta Watanzania pamoja, kuhamasisha ufugaji nyuki na kutuandaa
kuwa wenyeji bora wa mkutano mkubwa utakaotoa fursa za kiuchumi na kijamii,”
alisema Prof. Silayo huku akishukuru ushirikiano wa wadau na viongozi kutoka
mataifa jirani.
Rais wa Kamisheni ya
Afrika ya Apimondia, Bw. David Mukomana, alisema Nyuki Marathon ina ujumbe wa
kipekee unaopaswa kuenezwa ndani na nje ya Afrika, akisisitiza umuhimu wa
kulinda na kuhifadhi nyuki kama chanzo muhimu cha ajira na usalama wa chakula.
Mukomana alieleza kuwa
zaidi ya asilimia 70 ya vijana barani Afrika wanahitaji ajira na ufugaji nyuki
ni fursa muhimu ya kiuchumi. Pia aliongeza kuwa sekta hiyo inaweza kuchangia
kuongeza uzalishaji wa mazao na kupunguza uagizaji wa chakula.
Rais wa Apimondia
Duniani, Dk. Jeff Pettis, alipongeza Tanzania kwa maandalizi ya mkutano huo na
kueleza kuwa marathon hii ni jukwaa la kipekee la kuunganisha jamii katika kulinda
bioanuai na misitu asilia.
Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba,
alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuunga mkono juhudi za serikali katika
maandalizi ya mkutano huo na kuongeza thamani ya bidhaa za nyuki nchini.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Workers Bee Africa, Restituta Lopes Semedo, alisema Nyuki
Marathon inalenga pia kuondoa dhana potofu kuwa ufugaji nyuki ni shughuli ya
watu wa kipato cha chini pekee.
“Huu ni mwamko mpya.
Tunataka Watanzania waone nyuki kama hazina inayotoa asali, nta na bidhaa
nyingine zenye thamani kubwa duniani. Tunawahamasisha kuzingatia viwango ili
kuvutia masoko ya kimataifa,” alisema Semedo.
Mmoja wa washiriki wa
mbio hizo, Miriam Kileo kutoka Arusha, alisema: “Nimefurahi kushiriki Nyuki
Marathon kwa mara ya kwanza. Imenifanya nione kuwa ufugaji nyuki ni fursa
ambayo hata sisi vijana wa mijini tunaweza kuichangamkia na kupata kipato.”
Marathon hiyo
imewakutanisha washiriki kutoka nchi jirani zikiwemo Kenya, Zimbabwe, Burundi
na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, jambo linaloifanya kuwa tukio la kikanda
lenye lengo la kuunganisha sauti moja ya kulinda na kuendeleza ufugaji
nyuki barani Afrika.
0 Maoni