Katika tukio la
kihistoria lililojawa na hisia na shukrani, Shirika lisilo la kiserikali la
Foundation for Disabilities Hope (FDH) limemkabidhi Kamishna wa Uhifadhi wa
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA(T) Musa Nassoro Kuji tuzo
maalumu ya heshima yenye lengo la kutambua mchango mkubwa wa Shirika hilo
katika kukuza huduma jumuishi kwa makundi maalum nchini.
Akizungumza wakati wa
hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa FDH Bw.
Michael Salali alieleza kuwa TANAPA imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha
watu wenye ulemavu hawabaki nyuma katika kunufaika na vivutio vya utalii na
huduma jumuishi zinazopatikana ndani ya Hifadhi za Taifa nchini.
Alisema, “Upendo wenu
umefanya mabadiliko chanya na umechipua mizizi ya mafanikio yaliyojengwa
sanjari na nia yenu njema kwa watu wenye ulemavu.”
Aidha, Bw. Salali
aliongeza, “Tunatambua na kuthamini sana mchango wa TANAPA kwa watu wenye
ulemavu kwani umechangia na kuinua uchumi kupitia fursa mbalimbali ambazo
zimeendelea kutolewa na TANAPA.”
Vilevile, Mkurugenzi huyo
alisisitiza, “TANAPA ni shirika la mfano
wa kuigwa kwa kufanya huduma zake kuwa jumuishi, tunapokuja TANAPA tunajisikia
tuko nyumbani. Maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia katika kusaidia walemavu mnayaendeleza
kwa vitendo.”
Kwa upande wake Kamishna
wa Uhifadhi - TANAPA CPA (T) Musa
Nassoro Kuji alisema, “Kuweka mazingira rafiki na jumuishi kwa watu wote ndiyo
dhamira kuu ya TANAPA na tutaendelea kufanya hivyo kwa mustakabali wa Taifa letu.”
Aidha, hivi karibuni
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania lilipewa tuzo yenye mrengo huo kwa
kutambuliwa katika mchango wa watu wenye ulemavu kupitia Hifadhi za Taifa Gombe
na Mahale katika maonesho ya utalii
yaliyofanyika Kigoma mjini. Tuzo iliyokabidhiwa kwa Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassimu Majaliwa.”
Hafla hiyo ya utoaji wa
tuzo uliofanyika leo Julai 18, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa TANAPA uliopo
jijini Arusha umehudhuriwa pia na Makamishna Waandamizi akiwemo Naibu Kamishna
wa Uhifadhi - Massana Mwishawa, maafisa na askari pamoja na wawakilishi
waandamizi wa Shirika la Faoundation for Disiabilities Hope (FDH).
0 Maoni