Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema wakati umefika kwa
wanahabari wa Kiafrika kuonesha taswira nzuri ya Bara la Afrika kwa kuandika
habari chanya zenye nguvu na za kutia moyo kuhusu Bara hili.
Makamu wa Rais amesema
hayo wakati akifungua Mkutano wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika unaofanyika
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Amesema kwa kipindi kirefu
Bara la Afrika limekuwa likitegemea simulizi za vyombo vya habari vya nje ambazo
zimejikita katika hatari, vita, migogoro, na kushindwa huku vikipuuza uwezo
mkubwa, uthabiti, na maendeleo ya watu wa Afrika.
Amesisitiza umuhimu wa
kuwa na habari zinazoonyesha ushindi wa jamii za Kiafrika, wajasiriamali wa
biashara maarufu duniani, ubora wa kitaaluma wa wanafunzi wa Afrika, uvumbuzi
wa vijana, ujasiri wa wanawake na michango inayoongezeka ya Afrika katika
sayansi, teknolojia, utawala bora, na uchumi wa kimataifa.
Makamu wa Rais amesema ni
vema kuanza kuandika historia ya Bara hili kwa maneno na sauti ya Wafrika
wenyewe. Amesema Katika kuendeleza Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika, ambayo
inatazamia kuwa na bara lenye amani, umoja, ustawi na heshima ya kimataifa,
vyombo vya habari lazima vichukue jukumu la kuleta mabadiliko. Amesema ni
lazima kutumika kama daraja linalounganisha mataifa, kuwezesha mazungumzo yenye
maana katika Bara zima na kulinda utajiri wa urithi wa kihistoria na kitamaduni
wa Afrika kwa vizazi vijavyo.
Pia Makamu wa Rais ametoa
wito kwa washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabaraza Huru ya Habari kuandaa
mapendekezo ikiwemo ya kisheria au maeneo ambayo yanahitaji kuboreshwa ili
kutumia vyema manufaa ya Akili Unde (AI) katika tasnia ya habari.
0 Maoni