UWEKEZAJI mkubwa
uliofanywa na Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya nishati,
umeuwezesha Mkoa wa Tanga kuwa na hifadhi ya lita za ujazo milioni 210 za
mafuta ya petroli na dizeli.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga,
Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amesema hayo leo Julai 15, 2025, alipozungumza
na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Kikao hicho ni sehemu ya
utaratibu wa Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, kuwaalika Wakuu wa Mikoa
kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe Rais Dkt
Samia.
Mhe Balozi Dkt. Batilda
amesema, kiasi hicho cha mafuta kinachohifadhiwa kwenye tenki za mafuta za
kampuni ya GBP, kinakidhi matakwa ya kanuni za nishati hiyo na maagizo ya Mhe
Rais Dkt. Samia, kusambazwa kwenye mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na
Tanga.
Amesema usambazi wa
mafuta kutokea mkoani Tanga, kunachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za
usafirishaji kwa wafanyabiashara, hivyo bei kuwa rafiki kwa watumiaji.
Mhe Balozi Dkt. Batilda
amesema hifadhi hiyo ya mafuta, ni sehemu ya fursa nyingi za kiuchumi zilizopo
na zinazoendelea kukua mkoani Tanga, tangu Mhe Rais Dkt. Samia kuingia
madarakani 2021.
NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Mhe Balozi Dkt Batilda
amesema, Tanga inaendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia
kwa wananchi, taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali.
Kwa mujibu wa Mhe Balozi
Dkt. Batilda, hadi sasa taasisi 1,493 za Serikali zenye watumiaji 735,372 wa
nishati safi ya kupikia zimetambuliwa.
BOMBA LA MAFUTA GHAFI
Mhe Balozi Dkt. Batilda
amesema, Mradi wa Bomba na Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) wenye urefu
wa kilomita 205.91 unaohusisha ujenzi wa kituo cha kupokelea, kuhifadhi na
kusafirisha mafuta, usimamizi na uendeshaji wa mradi na matenki manne,
umekamilika kwa asilimia 53.
Amesema, fidia kwa wakazi
waliopisha mkuza wa EACOP mkoani Tanga umefikia asilimia 98.7 ambapo kati ya
wananchi 1560 kati ya wanufaika 1580 wameshapokea malipo ya fidia inayofikia
Shilingi billion 9.38.
Na. Mashaka Mgeta - Dodoma
0 Maoni