CHAMA cha Mtandao wa
Mabloga Tanzania (TBN) kimeshukuru uamuzi wa serikali ya kuwapatia mafunzo
maalumu ya kunoa weledi na uzalendo wa wanachama wake kuelekea uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Mabloga zaidi ya 200 wakiwemo wa diaspora
walioanzisha Mtandao huo mwaka 2015 watapata mafunzo hayo.
“Tumekuwa na mazungumzo
na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambao kimsingi ndio wasimamizi wakuu
wa maudhui na wametuthibitishia kwamba wapo hatua za mwisho za kutekeleza
maagizo ya serikali ya kutoa mafunzo kwa mabloga wote nchini,” alisema
Mwenyekiti wa TBN , Beda Msimbe.
Akifafanua kuhusu mafunzo
hayo, Msimbe alisema kwamba lengo kuu la mafunzo ni kuwajengea mabloga weledi,
uzalendo, na umakini katika kutambua na kupambana na habari feki, huku
wakiwezesha usambazaji wa taarifa sahihi zitakazowawezesha wananchi kufanya
maamuzi sahihi katika uchaguzi mkuu ujao.
“ Tunahitaji kukumbushana
kuhusu nchi hii, katiba yetu, amani na umuhimu wa uchaguzi katika demokrasia ya
aina yetu.Uamuzi huu wa serikali wa kutupiga msasa ni muhimu sana,” alifafanua.
Katika taarifa yake kwa
vyombo vya habari Mwenyekiti huyo wa TBN, Beda Msimbe, alieleza kuridhishwa na
juhudi zinazofanywa na serikali kufanikisha mafunzo. Alisema wameomba mafunzo
hayo kipindi cha sasa kwa kuwa wapo wanablogu ambao ni mara ya kwanza kuelekea
katika uchaguzi mkuu, na kurejea ombi lao tena wakati wa mkutano wa wadau
ulioandaliwa na Wizara ya Habari,Utamaduni,sanaa na michezo.
Alisema kwamba uongozi wa
TBN kwa sasa unafanya kazi kwa karibu na serikali kuhakikisha kuwa zaidi ya
wanachama 150 wa chama hicho waliotawanyika nchini kote wanafaidika kikamilifu
na mafunzo haya muhimu.
Msimbe aliwataka mabloga
wote nchini kuhakikisha wanawasiliana na Mratibu wa TBN, Bw. Gadiola Emanuel
ili kuthibitisha anwani zao na kuhakikisha taarifa zao ziko sahihi kwa ajili ya
ushiriki. Pia alitumia fursa hiyo kuwaalika wale wote ambao bado hawajajiunga
na TBN kufanya hivyo sasa ili waweze kunufaika na fursa hii muhimu ya mafunzo.
Chama cha Mabloga
Tanzania (TBN) kinajumuisha mabloga wanaotengeneza aina mbalimbali za maudhui,
ikiwemo michezo, habari za siasa, afya, uchumi, na habari mchanganyiko. Mafunzo
haya yanatarajiwa kuimarisha uwezo wao wa kutoa taarifa zenye ukweli na
uhakika, hivyo kuchangia katika mazingira ya uchaguzi yenye uwazi na
uwajibikaji.
0 Maoni