WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ametoa onyo kwa wasambazaji na wauzaji wa dawa za kulevya kwamba
Tanzania siyo mahali pa kufanyia biashara zao.
Waziri Mkuu ambaye
amefunga maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan amesema: “Tanzania siyo mahali salama kwa wauzaji, wasafirishaji,
walimaji na hata pia watumiaji wa dawa za kulevya. Tanzania tumeiva na sasa
tunaenda kukomesha biashara hii.”
Ametoa kauli hiyo jana
jioni (Alhamisi, Juni 26, 2025) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa
Dodoma wakiwemo wananchi, wadau, viongozi wa Serikali, wa dini na siasa ambao
walihudhuria kilele cha maadhimisho hayo kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya
Kikwete, jijini Dodoma.
“Makamishna na wakuu
wa vyombo vya ulinzi fanyeni kazi, imarisheni ulinzi iwe ni kwenye SGR, vituo
vya mabasi, bandari na viwanja vya ndege ili tuweze kuokoa vijana wetu. Dawa
hizi zina madhara makubwa kwani zinapoteza uwezo wa mwili na uwezo wa kiakili
wa kufikiri mambo,” amesisitiza.
Amesema kuwa
anatambua kwamba kuna mjadala ulioibuka baina ya wachumi na wadau wa kuzuia
matumizi ya dawa za kulevya huku wachumi wakidai kuwa zinaleta fedha na kuacha
kuangalia madhara ya kiafya ambayo wadau wanayasemea. “Kama tunataka tuwe na
kundi la vijana wa Kitanzania mazezeta, basi turuhusu hii biashara. Lakini,
Serikali hii tumekataa kwa sababu tunaamini kuwa hiyo mijadala haina tija na
hatutairuhusu,” amesisitiza Waziri Mkuu na kushangiliwa.
Amesema kazi kubwa ya
uwekezaji kwenye eneo hilo imefanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye
ameongeza bajeti ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
na kuwapatia vyombo vya usafiri ili wafanye kazi yao kwa ufanisi zaidi.
Akielezea kuhusu
ugumu uliokuwepo wa kuhitimisha kesi za watu waliokuwa wanakutwa na dawa hizo,
Waziri Mkuu amesema: “Lazima tulipongeze Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuruhusu Sheria ya Dawa za Kulevya itungwe; na hii ilikuwa ni
baada ya kubaini kulikuwa na mapungufu kwenye mfumo wetu wa sheria,” amesema.
Aliwaeleza washiriki
wa maadhimisho hayo kwamba kutokana na uwepo wa sheria hiyo, katika kila kesi
100 zinazofikishwa mahakamani, Serikali imeweza kushinda kesi 76.
Amesema ufanisi
mkubwa unaoonekana hivi sasa unatokana na kufungamanishwa kwa Mamlaka ya DCEA
ya Tanzania Bara na ile ya ZDCEA ya Zanzibar ambazo zinafanya kazi kwa karibu.
Mapema, akimkaribisha
Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki hao, Naibu Waziri wa Nchi (OWM – Sera,
Bunge na Uratibu) Ummy Nderianga alisema Rais Samia ameweka fedha nyingi na
vifaa ili kuhakikisha anawaokoa vijana wa Kitanzania kutoka kwenye matumizi ya
dawa za kulevya.
Amesema Ofisi ya
Waziri Mkuu imeongeza operesheni na usimamizi kwa kufungua ofisi za kanda
ambapo mkoa wa Dodoma tayari unayo ofisi ya Kanda.
Naye, Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mahmoud Thabit Kombo alisema kwenye
mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kimataifa Tanzania iko vizuri. “Tunakotokea
siyo hapa tulipo leo. Wakati ule, tulikuwa tunajulikana kama mapito ya dawa za
kulevya. Lakini chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania
tumeondoka kwenye doa hilo.
Kwa upande wake,
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alisema kutokana na uongozi madhubuti
wa Serikali ya awamu ya sita, kwa kipindi cha kuanzia Juni, 2024 hadi Mei,
2025, kumekuwa na ongezeko la ukamataji wa dawa za kulevya ukilinganisha na
miaka iliyopita.
“Katika kipindi hiki,
kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, tumekamata dawa za
kulevya jumla ya kilogramu 2,301,414.94. Kiasi hiki ni kikubwa ikilingalishwa
na kilo 2,050,542.73 zilizokamatwa kati ya Juni, 2023 na Mei, 2024. Kuanzia
Januari hadi Desemba 2024, jumla ya kilo 2,327,983.8 zilikamatwa ikilinganishwa
na kilo 1,965,341 zilizokamatwa kwa kipindi kama hicho
kwa mwaka 2023.”
0 Maoni