Shamba la Miti la
Meru-Usa, linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),
limeibuka kuwa mfano wa mafanikio katika uwekezaji na utendaji baada ya kuvuka
malengo ya uzalishaji, mapato, na idadi ya watalii kwa mwaka wa fedha
2024/2025.
Katika taarifa yake
kwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya TFS, iliyotolewa Juni 25, 2025, wakati wa
ziara ya siku mbili ya bodi hiyo (Juni 24–25), Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo,
Ali D. Maggid, alieleza kuwa mapato ya shamba hilo yamefikia Shilingi bilioni
4.4 dhidi ya lengo la Shilingi bilioni 3.5, ikiwa ni utekelezaji wa asilimia
122.
“Kupitia mkakati
madhubuti wa ukusanyaji mapato na uvunaji wa magogo ya thamani kubwa, tumevuka
makadirio ya mapato kwa zaidi ya Shilingi milioni 900. Tunajivunia kuwa sehemu
ya mabadiliko chanya ya uchumi wa sekta ya misitu nchini,” alisema Maggid.
Aidha, idadi ya
watalii wa ndani na nje imeongezeka kwa kasi, kutoka 7,300 mwaka 2021/2022 hadi
32,000 mwaka 2024/2025, na kuchangia zaidi ya Shilingi milioni 236 katika
mapato ya utalii wa ndani pekee.
“Eneo la Napulu
Waterfalls lililopo ndani ya shamba hili limekuwa kivutio kikubwa cha utalii wa
ikolojia, hasa kutokana na ukaribu wake na Jiji la Arusha. Hii imerahisisha kwa
wageni kuutembelea hata kwa muda mfupi wa jioni,” aliongeza Maggid.
Katika eneo la
uzalishaji wa miche, shamba hilo limesambaza miche 1,000,385 dhidi ya lengo la
miche 1,000,000, huku mbegu bora za miti zikitolewa kwa taasisi mbalimbali na
wananchi. Hata hivyo, changamoto ya matumizi yasiyo rasmi ya miche hiyo
imebainika, baadhi ya wananchi wakihusishwa na kuiuza kinyume na makusudio ya
upandaji.
Shamba hilo pia
limeanza ujenzi wa miundombinu muhimu ya utalii, ikiwemo ofisi, nyumba ya
walinzi, na jengo la huduma kwa gharama ya Shilingi milioni 171.6, ambapo kazi
hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo Julai 15, 2025.
Katika mchango wake
kwa jamii, Shamba la Meru-Usa limekuwa likisaidia vifaa vya ujenzi kwa shule,
zahanati, na ofisi za vijiji. Aidha, wananchi wa vijiji 32 vinavyozunguka
shamba hilo hupewa fursa ya kulima katika maeneo yaliyoandaliwa kwa ajili ya
upandaji mpya wa miti, hatua inayosaidia kuongeza uhakika wa chakula.
Kwa upande wake,
Mjumbe wa Bodi ya TFS, Enock Emmanuel Nyanda, Mkurugenzi Msaidi Idara ya
Uratibu wa Sekta Ofisi ya Rais TAMISEMI, alisisitiza umuhimu wa TFS kutumia
takwimu chanya za utendaji kama nyenzo ya kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi
kupitia majukwaa ya kitaifa kama Sabasaba na Nane Nane.
“TFS inapaswa kuwa
kinara wa kuonesha fursa za uwekezaji katika rasilimali za misitu, hasa maeneo
kama Meru-Usa yenye jiografia rafiki kwa utalii wa muda mfupi. Hili ni eneo la
kimkakati linalopaswa kuendelezwa zaidi,” alisema Nyanda.
0 Maoni