WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa zinaweka vituo vya kuchakata na kutenganisha taka ili zinapozalishwa ziweze kushughulikiwa kwa njia salama na endelevu, kwa lengo la kupunguza mzigo wa taka unaokwenda majalalani au kusambaa ovyo katika makazi ya watu.
Kadhalika, Mheshimiwa
Majaliwa amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa zishirikiane na Ofisi ya Makamu
wa Rais, Muungano na Mazingira kuandaa mipango ya kuwezesha jamii na vijana
kushiriki biashara ya kaboni, kutumia na kuendeleza teknolojia za nishati safi
na miradi ya urejelezaji wa taka (recycling).
Waziri Mkuu ametoa
maagizo hayo leo (Jumanne, Juni 03, 2025) alipozungumza na vijana katika Jukwaa
la Vijana na Mazingira lililofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani
ambayo hufanyika Juni 5 kila mwaka ambapo kitaifa yatafanyika Jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema
jukwaa hilo la vijana na mazingira linalenga kuwaunganisha vijana kutoka sehemu
mbalimbali nchini na kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya utunzaji wa mazingira
pamoja na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kubuni na kutekeleza mikakati
ya kutatua changamoto za mazingira nchini.
Amesema ni vizuri
uhamasishaji wa kuendeleza Kampeni ya Usafi wa Mazingira inayofanyika kila
Jumamosi ya mwisho wa mwezi uimarishwe kwa wananchi na jamii na sekta binafsi
nayo iweke mifumo ya urejelezaji wa taka zinazotokana na shughuli za viwanda
Ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa haziishii kuharibu mazingira.
“Tunavyoelekea
kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni, 2025, ni muhimu kwa vijana
kutambua nafasi yenu kwenye agenda ya mazingira kupitia jukwaa hili. Jukwaa
hili la vijana na mazingira linapaswa kuwa chachu ya kuibua ubunifu, kuongeza
uelewa na kushirikisha nguvu kazi ya Taifa katika kulinda na kuhifadhi
mazingira yetu.”
Akizungumzia kuhusu
mikakati ya Serikali ya kulinda mazingira, Waziri Mkuu amesema Serikali ya
Awamu ya Sita imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhamasisha matumizi
ya nishati safi ya kupikia ambapo zaidi ya taasisi 762 zimekwisha anza kutumia nishati
mbadala. Malengo ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi
kufikia mwaka 2034.
Amesema katika
upandaji miti, mwaka 2023/2024, zaidi ya miti milioni 266 ilipandwa, pamoja na
juhudi za kupanda miti bado Taifa linakabiliwa na changamoto ya upotevu wa
misitu inayokadiriwa kufikia hekta 469,420 kwa mwaka, ambapo Serikali
imefanikiwa kuweka msukumo katika ushiriki wa vijana katika shughuli za
mazingira.
“Usafi wa mazingira
na udhibiti wa taka ni moja ya changamoto za kimazingira zinazohitaji hatua za
makusudi na za haraka. Takwimu zinaonesha kuwa, takribani kiasi cha tani
millioni 14.4 hadi 20.4 za taka ngumu huzalishwa nchini hususani katika miji
mikuu na majiji. Aidha, ni wastani wa asilimia 50 tu ya taka zinazozalishwa
hukusanywa na kutupwa ipasavyo.
Amesema kutokana na
maendeleo ya sayansi na teknolojia, changamoto hizo ni fursa zinazoweza kutoa
ajira kwa vijana, kukuza uchumi na kuongeza kipato kwa kijana mmoja
mmoja. “Hivyo, nitumie fursa hii kuwasihi vijana wote mliopo hapa,
kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa
kuzingatia kuwa ni fursa ya kuongeza kipato na ajira kwa ujumla.”
Amesema tarehe 28
Mei, 2025, Serikali ya Tanzania na Japan ziliingia makubaliano ya ushirikiano
katika mpango wa pamoja wa uwekezaji katika biashara ya hewa ya ukaa (kaboni)
utakaoongeza fursa ya kupanua soko la biashara hiyo nchini. Aidha, Serikali
imenzisha kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa kaboni kupitia sheria ya
Usimamizi wa Mazingira iliyofanyiwa marekebisho ya Mwaka 2025. “Hii ni hatua
nyingine ya Serikali ya kusahirikiana na wadau wa mazingira.”
Kwa upande wake,
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamza Khamis
amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imeweka
jitihada kubwa za utunzaji wa mazingira ambapo imeelekeza kila halmashauri
kupanda miti isiyopungua milioni 1.5 kila mwaka.
Pia, Naibu Waziri
huyo amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuibua fursa
zitokanazo na masuala ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira kama biashara ya
kaboni, urejeshaji wa taka pamoja na kuandaa kanuni, mikakati na miongozo
mbalimbali ya usimamizi wa mazingira ukiwemo muongozo wa 3R yaani punguza,
tumia tena na rejeleza wenye lengo la kuimarisha na kusimamia taka nchini.
“Tulikuwa tunasema
taka ni uchafu ila sasa taka ni utajiri na taka ni suluhisho la vijana
kwenye mazingira.”
0 Maoni