Maandamano kila kona kumpinga Rais Trump

 

Miji na Majiji mbalimbali nchini Marekani imeshuhudia maandamano makubwa dhidi ya Rais Donald Trump, maandamano ambayo yameandaliwa na kikundi kijulikanacho kama "No Kings".

Waandamanaji hao walijitokeza kwa wingi kupinga gwaride la kijeshi lililoandaliwa jijini Washington DC, tukio ambalo ni nadra kufanyika, na lilifanyika sambamba na siku ya kuzaliwa kwa Trump.

Gwaride hilo pia lililenga kuadhimisha miaka 250 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Marekani.

Maandamano hayo yamekuja baada ya wiki ya maandamano makubwa yaliyofanyika Los Angeles na maeneo mengine, watu wakilalamikia sera kali za uhamiaji za utawala wa Rais Trump.

Katika majiji kama New York, Philadelphia na Houston, wabunge, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wanaharakati mbalimbali walihutubia umma uliojumuika kwa maelfu huku wakipeperusha bendera za Marekani na mabango yenye ujumbe mkali wa kumpinga Trump.

Katika onyo kali kabla ya gwaride hilo lililofanyika Jumamosi jioni, Rais Trump alitahadharisha kuwa maandamano yoyote yangekabiliwa na "nguvu kubwa".

Chapisha Maoni

0 Maoni